1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kisiasa nchini Yemen imeendelea kuwa tete

27 Mei 2011

Hali nchini Yemen inaendelea kuwa tete, huku wapinzani wa kiongozi Ali Abdallah Saleh na wanaomuunga mkono wakijiandaa kufanya maandamano leo baada ya wiki moja ya mapigano makali.

https://p.dw.com/p/11P8X
Polisi wakisafisha barabara baada ya kuwatawanya waandamanajiPicha: AP

Katika hatua nyingine viongozi wa nchi za G8 waliyopo katika mkutano wa mataifa yenye nguvu duniani huko nchini Ufaransa wanasema kiongozi huyo lazima aondoke madarakani.

Zaidi ya wayemeni 40 waliuwawa jana katika mji wa Sanaa katika siku ya nne ya mapigano tangu kukiukwa kwa makubaliano ya wengi ya kumtaka rais Ali Abdallah Saleh kuondoka madarakani.

Ijumaa imekuwa siku ya maandamano ya wapinzani na wanaomuunga mkono rais huyo, ambaye tangu uongozi wake, nchi hiyo imeendelea kuwa maskini, katika eneo hilo la nchi zenye mafuta.

Maelfu ya wananchi wamekuwa wakikimbia mapigano hayo na wengine kuishi kwa hofu, nchini humo.

Mapigano hayo baina ya majeshi ya Ali Abdallah Saleh na wanachama wa kundi la kabila la Hashed linaloongozwa na Sadiq al-Ahmar, yamesababisha umwagaji damu mkubwa tangu upinzani nchini humo kuanza Januari mwaka huu.

Zaidi ya watu 80 wameuwawa tangu Jumapili iliyopita. Milio ya risasi imesikika katika mji wa Sanaa jana na milio ya mabomu katika eneo ambalo maelfu ya watu wanaomtaka kiongozi huyo kuachia madaraka, wameweka kambi.

Upinzani nchini humo, ulitumia tovuti mbalimbali kwenye mtandao wa intaneti na simu kuitisha maandamano ya amani ya kuleta mageuzi nchini humo.

Ujumbe mmoja wa simu ulisema maandamano hayo ni ya kusisitiza mageuzi ya amani na kukataa juhudi za kuingiza nchi hiyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Viongozi wa kabila la Ahmar wakiwemo, Sadiq al Ahmar na Hamid al-Ahmar, wanawaunga mkono wapinzani.

Ali Abdullah Saleh / Jemen / Präsident
Rais wa Yemeni Ali Abdulla SalehPicha: AP

Wanaomuunga mkono kiongozi Ali Abdallah Saleh nao wameandaa maandamano yao, waliyoyaita 'Ijumaa ya sheria na Amri' yatakayofanyika karibu na maandamano ya wapizani.

Nao pia wanatumia ujumbe mfupi wa simu unaolaani vitendo vya 'uhalifu dhidi ya haki na uasi dhidi ya nchi'.

Kuna wasiwasi kuwa nchi ya Yemeni ambayo tayari uchumi wake umeporomoka kutokana na vurugu hizo, inaweza kuwa nchi iliyoshindikana, ambayo itakuwa hatari kwa usalama wa nchi jirani kama Saudi Arabia.

Marekani na Saudi Arabia nchi ambazo zimekuwa shabaha ya kundi la ugaidi la Al Qaeda kutokea kituo chao nchini Yemen, zina wasiwasi kuwa kutokuwepo na serikali nchini humo kutaipa nafasi kubwa kundi hilo kuendeleza ugaidi.

Viongozi wanaohudhuria mkutano wa G8 nchini Ufaransa wamelaani nguvu kali inayotumiwa na majeshi ya serikali nchini Yemen, dhidi ya wapinzani na kumtaka rais Ali Abdallah Saleh awe mwaminifu na kuhitimisha uongozi wake wa miaka 33.

Viongozi hao wametoa wito wa mabadiliko ya amani nchini humo.

Mwandishi: Rose Athumani/Reuters

Mhariri:Josephat Charo