1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Habeck ziarani Mashariki ya Kati

Mohammed Khelef
6 Juni 2022

Naibu Kansela wa Ujerumani, Robert Habeck, anaanza ziara katika eneo la Mashariki ya Kati kuzungumzia masuala ya vyanzo vya nishati salama na pia kuzorota kwa hali ya usalama katika eneo hilo katika siku za karibuni.

https://p.dw.com/p/4CKmF
Robert Habeck I Kongress in Berlin
Picha: Political-Moments/IMAGO

Kituo cha kwanza cha naibu kansela huyo wa Ujerumani, ambaye pia anashikilia wadhifa wa waziri wa uchumi anayehusika na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, ni nchini Israel, ambako anawasili hivi leo mjini Jerusalem anakokutana na wawakilishi wa serikali ya Israel kuzungumzia masuala ya kiuchumi na kisiasa. 

Kikao hicho pia kitajikita kwenye ushirikiano baina ya Ujerumani na Israel katika mambo ya nishati, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia, msisitizo ukiwekwa kwenye nishati jadidifu.

Kuna kiwango kikubwa cha gesi asilia kando mwa fukwe za Israel na Ujerumani kwa sasa inajaribu kusaka vyanzo vipya vya nishati. Wakati mashambulizi ya Urusi yakiongezeka nchini Ukraine, Ujerumani inajaribu kujikwamua kwenye utegemezi wake kwa gesi ya Urusi.

Kabla ya kuondoka mjini Berlin, Habeck aliwaambia waandishi wa habari kwamba hata kama suala la vyanzo vipya vya nishati kwa nchi yake sio kiini cha ziara hiyo, lakini ukweli unasalia kwamba Ujerumani itakuwa na upungufu wa gesi kama itaachana na gesi ya Urusi.

Mipango ya gesi ya Israel

Kumekuwa na mipango ya kujengwa bomba la gesi kupitia Bahari ya Mediterenia kuingia Ulaya, ambayo kama itakamilika itaweza kusafirisha gesi kutoka Israel kupitia Cyprus hadi Ugiriki na kwa hivyo kwa Umoja wa Ulaya.

Lakini Habeck alisema kusafirisha gesi kuingia Ulaya hakutakuwa rahisi sana kutokana na upungufu wa miundombinu.

Kesho, Jumanne, Habeck atatembelea maeneo yaliyo chini ya Mamlaka ya Palestina na Jordan, ambako atashiriki kongamano la nishati baina ya Jordan na Ujerumani. 

Ziara ya naibu kansela huyo wa Ujerumani, inafanyika wakati kukiwa na wimbi la ghasia zilizopelekea vifo ndani ya Israel na Mamlaka za Palestina tangu mwezi Machi.

Kuuawa kwa mwandishi wa habari wa Al Jazeera, Shireen Abu Akleh, wakati wa operesheni ya kijeshi na matumizi ya mabavu ya polisi wa Israel katika mazishi yake yameongeza makali ya mzozo huo. 

"Kuna hali mbaya sana ya wasiwasi baina ya Israel na Mamlaka za Palestina, vifo vingi, mashambulizi mengi ya makundi ya kigaidi ya Palestina ndani ya Israel, operesheni za wanajeshi wa Israel au vikosi vya usalama ndani ya mamlaka za Palestina na Jerusalem."

Alisema mwanasiasa huyo wa Ujerumani akiongeza kuwa lengo lake hasa ni kulirejesha suala la kukomesha machafuko katika mjadala kwa jinsi ambavyo Ujerumani inaweza.