1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Google yaizuia Huawei kutumia programu zake

Sudi Mnette
20 Mei 2019

Kampuni ya Google ya Marekani, ambayo inaendesha mfumo wa simu za mkononi wa Android karibu duniani kote imesema imeanza kusitisha uhusiano wake na kampuni ya Kichina ya Huawei kutoka na kitisho cha usalama.

https://p.dw.com/p/3IluG
Paraguay Google Play Store und Huawei Logo
Picha: picture-alliance/ZUMA Wire/A. M. Chang

Hatua hiyo itakuwa na athari kubwa kwa wenye kutumia simu za mkononi za Huawei, pale ambapo kampuni hiyo itakapokuwa haizipati tena huduma zinazomilikiwa na Google, ambazo zinajumuisha Gmail - anuani ya barua pepe na Google Maps - programu ya kuonesha ramani na muelekeo.

Katika kipindi hiki kilichogubikwa na vita vya kibiashara kati ya China na Marekani, Rais Donald Trump ameyazuia makampuni ya Kimarekani kujihusisha na biashara ya mawasiliano ya simu na mataifa ya kigeni, akisema inatishia usalama wa Marekani. Hatua hiyo inailenga kampuni ya Huawei, kama kampuni ya pili duniani kwa utengenezaji wa simu aina za "smart phone", ambayo ipo katika orodha ya kitengo cha biashara cha Marekani, ikiwa miongoni mwa kampuni ambayo, mashirika ya Marekani yanaweza kushirikiana nayo kibiashara endapo yatapata ridhaa kutoka serikalini.

Google inazingatia athari kwa wateja wake

Google-Logo in Beijing
Picha: Reuters/T. Peter

Marafuku hiyo inahusu mabadilishano ya teknolojia. Msemaji wa kampuni ya Google aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba "Tunazingatia amri na tunaitahimini athari zake kwa watumiaji wetu. Nyenzo ya kujikinga kutoka katika programu ya Google Play itaendelea kufanya kazi ya kukizuia kifaa chochote cha Huawei." Kwa kawaida Google, kama ilivyo kwa makampuni mengine ya kiteknolojia, yanawasiliana moja kwa moja na watengenezaji wa simu hizo za "smartphone" kwa lengo la kuhakikisha mfumo wake unawiana na vifaa wanavyotengeneza.

Kutokana na marufuku hii ya sasa, Google itasimamisha mwenendo wa kibiashara na Huawei, ambao unahusisha moja kwa moja usafirishaji wa vifaa na programu za kompyuta na huduma za kiufundi ambazo kwa kawaida haizitolewi kwa umma. Kwa maana hiyo, Huawei kwa sasa wataweza kutumia App ya Android tu, ambayo haitakuwa na huduma za Google.

Huawei na yatangaza namna ya kujinusuru na athari

Hata hivyo kampuni ya Huawei imesema itaendelea kulifanyia kazi suala la usalama na huduma katika simu zake na vifaa vingine vinavyozuiwa na Google, ingawa haijaweza wazi nini kinaweza kutokea kwa simu kwa simu ambayo zimekuwa zikitumia programu maarufu ya Google zikiwemo Gmail, You Tube na Crome.

Huawei ambayo kwa hivi sasa inaongoza katika teknolojia yake ya 5G, na simu zake aina ya smartphones, imeweza kuipiku sokoni kampuni ya Kimarekani ya Apple, iPhone, katika kipindi cha robo ya kwanza cha mwaka huu, kwa kuipora kampuni hiyo ya Califonia nafasi ya pili, zikiwa zinajongelea kwa karibu zaidi katika soko la smartphone ambalo linatawaliwa na Samsung.

Kwa upande wake, wizara ya mambo ya nje ya China imesema, China itaendelea kuyaunga mkono makampuni yake na itatumia silaha ya kisheria kwa lengo la kufanikisha azma hiyo. Vita vya kibiashara kati ya China na Marekani vya mapema mwezi huu, ilishuhudiwa Rais Trump akiongeza ushuru wa dola tahamni ya dola bilioni 200 kwa bidhaa zinazoingia nchini mwake kutoka China. Na China ikajibu mapigu kwa kuongeza kodi ya dola bilioni 60 kwa bidhaa za Marekani.

Vyanzo: RTR/DPA/AFPE