Marekani yaipiga marufuku Huawei | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yaipiga marufuku Huawei

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza hali ya dharura inayolenga kulinda mitandao ya mawasilinao ya taifa hilo

Rais Donald Trump ametia sahihi amri ya rais inayopiga marufuku ununuzi ama matumizi ya vifaa kutoka kwa kampuni ambazo zinatishia usalama wa taifa hilo na usalama wa raia wa Marekani.

Afisa mmoja mwandamizi kutoka ikulu ya White House amesema hakuna nchi wala kampuni maalum zilizolengwa na amri hiyo, huku msemaji wa ikulu Sarah Sanders akisema serikali ya Trump itafanya iwezavyo kuifanya Marekani salama na vile vile kuilinda dhidi ya maadui wakigeni.

Amri hiyo ya rais imeipa nguvu wizara ya biashara ya Marekani kuzuia kampuni za kimarekani kufanya biashara na kampuni kadhaa za kigeni. Japo tangazo hilo halijaitaja moja kwa moja kampuni ya Huawei ambayo ni kampuni kubwa katika kutoa huduma za mtandao wa kasi zaidi wa 5G lakini amri hiyo inatafsiriwa kwamba imeilenga kampuni hiyo.

Marufuku hii inajiri wakati Marekani na China ziko katika mvutanao wa kibiashara, hivyo basi imeonekana kwamba Marekani imechukua uamuzi huo kutokana na wasiwasi wake mkubwa wa kuwa kampuni ya Huawei inatumika na serikali ya China kuipeleleza Marekani.

Ajit Pai Netzneutralität USA (picture-alliance/AP Photo/J.Martin)

Kamishna wa idara ya mawasiliano wa Marekani (FCC) Ajit Pai

Kamishna wa idara ya mawasiliano wa Marekani (FCC) Ajit Pai amekaribisha amri hiyo ya rais Trump na kukubali kwamba walengwa ni China. Akizungumza na shirika la habari la Fox amesema kuna haja ya wao kuwa na taswira wazi ya vitisho vinavyowaelekea na kwamba amri hiyo inaonyesha wanavichukuliwa vitisho hivyo kwa makini sana.

Kampuni ya Huawei imetoa taarifa yake ikisema kwamba kuiwekea vikwazo kampuni hiyo kufanya biashara haitofanya Marekani salama wala kuipa nguvu bali ni kutumia njia zinazowagharimu pakubwa kujitoa uoga na vile vile kuifanya Marekani kubakia nyuma katika mtandao wa kasi wa 5G ambapo hapo itadhuru kampuni na raia wa Marekani wanaosubiri huduma hiyo.

Hauwei iko tayari kwa mazungumzo na Marekani

Zaidi taarifa hiyo inasema vikwazo visivyokuwa na sababu vitahujumu haki za kampuni ya Huawei na hivyo kuanzisha maswala mazito ya kisheria. Hata hivyo Huawei katika taarifa yake hiyo imesema kwamba iko tayari kuzungumza na serikali ya Marekani na kukubaliana kubuni mbinu bora zitakazowahakikishia usalama wa bidhaa zake.

Wizara ya biashara Marekani tayari imeiweka Huawei katika orodha mabaya hatua inayofanya iwe vigumu zaidi kwa kampuni hiyo kutumia vifaa muhimu vya Marekani katika simu na vifaa vyengine vya kieletroniki.

USA Bundesausschuss für Kommunikationen (picture-alliance/AP Photo/A. Harnik)

Ofisi za idara ya mawasiliano wa Marekani (FCC)

Awali Marekani ilizizuia taasisi za serikali kuingia katika mkataba na Huawei na kampuni nyengine zinazotumia vifaa vya Huawei kutokana na wasiwasi kwamba Huawei itatumia uwezo wake wa kutoa huduma ya 5G kupeleka taarifa kwa idara za kijasusi za China. Marekani pia ilitaka mataifa rafiki katika bara Ulaya pia kukata uhusiano na Huawei.

Idara ya mawasiliano FCC inasema wiki jana iliinyima China nyenzo za mawasiliano ya simu ya Marekani ili kuuanza kutoa huduma za simu Marekani ikisema kampuni hiyo inayomilikiwa na serikali ya China ni tishio kwa usalama.

Marekani na China wapo katika mvutano wa kibiashara ulioanza baada ya China kujitoa katika makubaliano ya biashara kubwa yaliyokuwa katika hatua za mwisho, China ilikiuka baadhi ya maagano yaliyokuwa yameafikiwa kwa kipindi cha miezi kadhaa cha mazungumzo hayo jambo lililosababisha mazungumzo hayo kuvunjika, kulingana na Trump.

(DPAE/AFPE)

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com