G-8 haisaidii Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.07.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

G-8 haisaidii Afrika

Kundi la nchi 8-tajiri (G-8) haliwezi kuisaidia Afrika.

Upatu unaopigwa kila kwa mara na kundi la nchi 8-tajiri kabisa ulimwenguni-G-8 ni porojo tupu-dawa isiotibu maradhi ambayo dola zinazoshiriki mkutanoni zamudu kuahidi kwa fedha kidogo tu na kuutia ulimwengu kitunga cha macho.

Kwa njia hii, dola hizo tajiri zaonesha huruma kwa maafa na madhila ya wanadamu ulimwenguni, kwa wale wenye kufa na njaa mbali mno na vituo vyao vya kifahari vya mikutano kama vile: Glenn Eagels,Heiligendamm na sasa Toyako,Japan. Na kila kundi hili la G-8 linapokutana, haliisahau mada yake hii maarufu: "msaada zaidi kwa Afrika"

Mada hii ya kuisaidia Afrika, si taabu kuingiza katika ajenda ya mkutano huu wa kilele wa G-8,kwani haigharimu kitu.Isitoshe, haisababishi ugomvi wala mvutano miongoni mwa viongozi wanaoshiriki kinyume na mada kama vile ulinzi wa mazingira na nishati ya nuklia.Kuahidi kuisaidia Afrika, yatosha kutoa ahadi za maneno matupu ambazo ama hazitimizwi kabisa au kwa ruzuku ndogo tu.

hii ni tabia na desturi ambayo mbali na mashirika ya misaada ni kiongozi mmoja tu inayomkera:Rais George Bush wa Marekani.

Na hiki ni kiroja cha mambo cha kundi hili la G-8 kusadifu George Bush kati ya wote ndie anaejitokeza kuliokoa bara la Afrika kana kwamba kwsa kujitolea kulisaidia kwa dala milioni kupiga vita ukimwi na Malaria mwishoni mwa kipindi chake cha utawala, kutaokoa awamu yake ya urais kukumbukwa kwa mema.

George Bush pekee leo hana uwezo wa kuuokoa mkutano wa kilele wa kundi hili la nchi tajiri za G-8 na la kimsingi zaidi na la kutanabahi ni hili:Hakuna mkutano wa kilele wa G-8 unaoweza kuikoa Afrika.

Ile dhana kuwa msaada zaidi wa maendeleo kutoka kundi hili la nchi 8-tajiri kuna maana maendeleo zaidi na kutapunguza upungufu wa chakula barani afrika,ni upumbavu.

Kwani, mfano wa Zimbabwe ,unadhihirisha maafa halisi yalioliangukia bara la Afrika: Bara la Afrika sio linaathirika kutokana na ukosefu mkubwa wa misaada ya maendeleo,bali na kuwa na viongozi wengi katika maqasri ya marais wanaohilikisha umma wao. Hawa ni viongozi ambao bila ya kuchelewa wastahiki kufikishwa mbele ya Mahkama Kuu mjini The Hague,Uholanzi kujibu madhambi yao dhidi ya binadamu wenzao.Kwani, Zimbabwe ni kama kuingia motoni ungali duniani,lakini sio kwa sababu viongozi wa dola kuu 8 hawatimizi ahadi zao za msaada wa kweli kwa Afrika,bali kwa kuwa jirani yake-Afrika Kusini, ndie anaemtia jeki Mugabe,tangu kifedha,silaha na kwa wataalamu wa mafunzo ya kijeshi.

Ethiopia, haifii kwa njaa kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa mbegu au kwa kuwa wakulima wa Marekani wanatumia mazao mengi ya chakula kutengezea nishati ya bio.

La, ni kwa kuwa mtawala wake anapenda mno vita visivyo na maana na kuligharimia jeshi lake hili kubwa barani Afrika kwa fedha.Eritrea,jirani yake, imepigania ukombozi na sasa rais wake anawapiga vita wananchi wake.

Kenya, yaweza kugeuka pepo ya kimaumbile

kwa watalii,lakini baadhi ya viongozi wanahiyari kuifisidi nchi na kuchochea kabila moja dhidi ya jengine.

Sehemu kubwa ya matatizo ya Afrika inatokana na waafrika wenyewe.Kwahivyo, hakuna mkutano wa kilele wa kundi la -G-8,utaoweza kuinusuru Afrika.Isipokuwa,viongozi wanaoshiriki, wanabadili ghafula nia na kukabili kwa nia safi tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaliathiri mno bara la Afrika.Lakini, hii haitatokea ,badala yake hata kwenye kikao kijacho cha kundi hili la G-8 utaisikia tena mada hiyo ya "kulisaidia bara la Afrika" ingawa ni porojo tupu.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com