1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
FIFA WM 2022  | Spanien - Deuschland
Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance
MichezoUjerumani

Flick: Hatufikiri sana kuhusu ubingwa wa mashindano ya EURO

13 Machi 2023

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Hansi Flick anataka kuona mabadiliko katika kikosi chake baada ya timu hiyo kuondolewa katika hatua ya makundi kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA nchini Qatar.

https://p.dw.com/p/4OcHY

Flick hata hivyo, amekataa kuitaja Ujerumani kama moja ya timu zenye uwezo wa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Ulaya EURO yatakayofanyika Ujerumani mwaka ujao 2024.

Akizungumza katika mahojiano katika toleo la Jumatatu la jarida la michezo la Kicker, na gazeti la Süddeutsche, kocha huyo wa timu ya taifa ya Die Mannschaft amekiri kufanya makosa ya kiufundi wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia, na kuongeza kwamba kuna masomo ambayo wanapaswa kujifunza kufuatia matokeo mabaya ya timu hiyo ya taifa.

Flick pia ameeleza kuwa mjadala juu ya uvaaji wa kitambaa cha One Love cha kupigania haki za wapenzi wa jinsia moja, ulikuwa na athari hasi kwenye maandalizi ya kikosi hicho.

Kocha huyo anaanza maandalizi ya mashindano ya EURO kwa mechi za kirafiki dhidi ya Peru mnamo mwezi huu wa Machi kabla ya kuteremka tena dimbani kuchuana na Ubelgiji siku chache baadaye.

"Katika hatua tuliyofikia, sisemi kama tuna uwezo wa kuchukua ubingwa wa EURO. Hakuna hakikisho juu ya hilo. Tunatoa hakikisho la kujitolea ili tuingie kwenye mashindano hayo wakati tumejiandaa kwa njia bora zaidi,” Flick ameiambia Kicker.

"Bila shaka tunataka tuwe na mafanikio. Kimsingi, nina malengo makubwa. Lakini tunapaswa kuwa wanyenyekevu, utatufaa sana. Kwanza kabisa, ni kufanya kazi za msingi.”

Soma pia: Maoni: Ujerumani sio timu ya juu tena

Flick anatarajiwa kutangaza kikosi chake cha kwanza baada ya Kombe la Dunia mnamo siku ya Ijumaa. Amesema ananuia kufanya majaribio katika mechi za kujipima nguvu za mwezi Machi na Juni kabla ya kusuka kikosi cha mwisho kwa ajili ya mashindano ya EURO kutoka mechi za Septemba.

Ameweka wazi kuwa, hatomjumuisha kikosini mshambuliaji mkongwe wa Bayern Munich Thomas Müller katika mechi mbili zijazo za kirafiki, japo haimaanishi kuwa amemfungia nafasi ya kuitwa kikosini katika siku zijazo. Kiungo wa Manchester City Ilkay Gündogan pia huenda asijumuishe kwenye kikosi cha timu ya taifa katika mechi za kirafiki dhidi ya Peru na Ubelgiji.