Diplomasia ya rais Mbeki kuhusu Zimbabwe yatiliwa shaka | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Diplomasia ya rais Mbeki kuhusu Zimbabwe yatiliwa shaka

Mjadala umeanza miongoni mwa wachambuzi na watetezi wa jamii za kiraia kuhusu jinsi rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini anavyotakiwa kuipatanisha serikali ya Zimbabwe na viongozi wa upinzani nchini humo.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini

Matumaini ni kwamba mazungumzo baina ya rais Thabo Mbeki na makundi ya kisiasa nchini Zimbabwe yataitanzua mizozo ya kisiasa na kiuchumi nchini humo ambayo imesababisha ukiukaji wa haki za binadamu, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira na ukosefu wa bidhaa muhimu.

Wengi wanahoji ikiwa hatua ya rais Mbeki kutumia diplomasia ya kunyaa kimya kuhusu mzozo wa Zimbabwe itafaulu. ´Rais Mbeki ameshindwa katika sera yake ya diplomasia ya kunyamaza kimya,´ amesema Idai Zimunya, mratibu wa muungano wa kukabiliana na mizozo nchini Zimbabwe, Crisis Coalition of Zimbabwe. Hii ni mara ya tano jumuiya ya SADC kumpa mamlaka ya upatinishi nchini Zimbabwe tangu mwaka wa 2000, ameongeza kusema Idai Zimunya.

Lakini Claude Kabemba wa shirika linalopigania jamii huru kusini mwa Afrika, Open Society Initiative, lililo na makao yake makuu mjini Johannesburg, amesema ni mapema kumhukumu rais Thabo Mbeki kwa kuzingatia alivyoshindwa katika majukumu ya awali. Claude Kabemba anadhani rais Mbeki anatakiwa kuondokana na sera yake ya kunyamaza kimya na aanze mazungumzo ya wazi ili watu wajue anachokifanya.

Mratibu huyo ameongeza kusema na hapa ninamnukulu, ´Zamani hatukujua alikuwa akizungumza na nani na hakuna aliyejua aliyekuwa akisababisha matatizo kwa diplomasia ya kunyamaa kimya. Ikiwa upatanishi unafanywa kwa uwazi watu watajua ni nani anayeutatiza,´ mwisho wa kumnukulu.

Kwa upande wake serikali ya Afrika Kusini inahoji kwamba sera ya kuzungumza wazi kutaitenga serikali ya rais Robert Mugabe na kusababisha maofisa wa Zimbabwe kuzidisha msimamo wao.

Mkutano wa jumuiya ya SADC mjini Dar es Salaam Tanzania, ambapo wanachama 14 wa jumuiya hiyo walimpa rais Thabo Mbeki kibarua cha kuutanzua mgogoro wa Zimbabwe, uliitishwa kufuatia wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa kuhusu kuzuka wimbi lengine la machafuko ya kisiasa nchini Zimbabwe.

Katika taarifa yake iliyotolewa tarehe 28 mwezi uliopita, shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, lenye makao yake mjini New York Marekani lilisema serikali ya Zimbabwe imeruhusu vikosi vya usalama kufanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa kuwatandika watetezi wa upinzani na raia wa Zimbabwe. Vikosi vya usalama vilihusika kuwakamata, kuwazuilia na kuwapiga wafuasi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, watetezi wa jumuiya za kiraia na wananchi kwa jumla.

Wiki iliyopita, maiti ya mpigaji picha wa Zimbabwe, Edward Chikomba, ilipatikana yapata kilomita 50 magharibi mwa mji mkuu Harare baada ya kutekwa nyara mwishoni mwa mwezi uliopita. Mauaji ya mtangazaji huyo wa zamani wa serikali yalisababishwa na hatua yake ya kuvipa vyombo vya habari vya kigeni picha zilizoonyesha majeraha aliyoyapata kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai, alipopata kipigo cha polisi wakati wa mkutano wa maombi mnamo tarehe 11 mwezi uliopita mjini Harare.

Kwa mujibu wa sheria ya kupata habari na kulinda haki ya kutoingiliwa ya mwaka wa 2002, waandishi wa habari wa kigeni wamefukuzwa nchini Zimbabwe na serikali imeifanya kuwa sheria waandishi nchini humo wajiandikishe.

Maaskofu wa kikatoliki nchini Zimbabwe wamesema ili kumaliza umwagikaji wa damu, nchi hiyo inahitaji katiba mpya itakayoielekeza kufikia utawala wa kidemokrasia utakaochaguliwa katika uchaguzi huru na wa haki. Aidha wamesema watatumia njia nyengine kuziongezea nguvu juhudi za SADC wakiamini kuwa si ufunguo pekee wa kuumaliza mzozo wa Zimbabwe.

 • Tarehe 10.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGf
 • Tarehe 10.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGf

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com