Bunge la Ujerumani lakubali wanamaji wa Kijerumani wapekekwe katika bahari ya Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bunge la Ujerumani lakubali wanamaji wa Kijerumani wapekekwe katika bahari ya Somalia

Wanamaji wa Ujerumani watapambana na maharamia wa meli huko Somalia

Wanamaji wa Kijerumani katika Pembe ya Afrika

Wanamaji wa Kijerumani katika Pembe ya Afrika

Kama tulivotaja mwanzo, Bunge la Ujerumani leo limekubali kutumwa wanamaji wa Kijerumani hadi Pembe ya Afrika. Wanajeshi hao pia watakuwa na uwezo wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya maharamia wa meli wanaoendesha shughuli zao katika mwambao wa Somalia. Lakini jambo hilo halitarajiwi litaisaidia dola hiyo ya Somalia iliosambaratika. Nchi hiyo inakosa suluhisho la kisiasa.

Andrew Mwangura ni mtu jasiri, na hivi sasa ni mtu anayetakiwa sana kohojiwa na vyombo vya habari, kama bingwa wa masuala ya uharamia wa meli. Si muda mrefu uliopita alikamatwa na wakuu wa usalama wa nchi yake ya Kenya, kwa vile hadharani alielezea wasiwasi kama vile vifaru vya kijeshi vilivokuwemo ndani ya meli ile ya Ukraine iliotekwa nyara katika mwambao wa Somalia vilikuwa kweli kwa jeshi la Kenya na sio, kama vile ilivochukuliwa na watu wengi, kwamba vilikusudiwa kwenda Kusini mwa Sudan. Vipi mkasa huo unahusiana na majadiliano juu ya kutumwa wanamaji wa Kijerumani katika Pembe ya Afrika? Na unahusiana vipi na uamuzi wa leo bungeni ambao unawapa uwezo wanamaji hao kutumia nguvu za kijeshi wanapowasaka maharamia katika mwambao wa Afrika?

Katika wiki ile iliopita, pale baraza la mawaziri la Ujerumani lilipochukuwa uamuzi huo, Andrew Mwangura alitoa tamko la kijasiri kabisa, nalo ni kwamba inahitaji kuliko manuwari za kivita kulimaliza balaa hili la maharamia wa meli katika mwambao wa Somalia. Hivyo, mwananchi huyo wa Kenya alitia chumvi kwenye kidonda. Mlolongo wa manuwari za ile Operesheni ilioanzishwa na Marekani, kwa jina la Operation Enduring Freedom, zile za Jumuiya ya Kijihami ya NATO na za kitaifa unaweza kuwafukuza maharamia. Ikiwa shehena za misaada kwa ajili ya Somalia mwishowe zitaweza kuwasili Mombasa, hilo, bila ya shaka, litakuwa ni fanikio. Lakini hiyo sio kwamba tatizo litaondoka. Maharamia hao wanahamishia zaidi vituo vyao vya operesheni upande wa Kusini. Huko, kwa mfano, kikosi cha Ujerumani kwa sasa hakitakiwi kupiga doria.

Mazungumzo ya sasa kuhusu uharamia wa baharini yamechomoza kwa muda mfupi sana, na, kwa sehemu, yanachukuwa sura ya ajabu. Jumuiya ya wamiliki wa meli za abiria inataka manuwari za Kijerumani ziwe tayari kuisindikiza kila meli. Na jee, vipi, baadae itakuwa watungaji shabaha wa Kijerumani watatakiwa wawasindikize watalii wa mazingira huko Afghanistan ya Kaskazini?

Kile kinachokihitaji huko Somalia sio kila wakati vikosi vipya vya manuwari katika mwambao wake. Kile ambacho nchi hiyo inahitaji, na jambo hilo linaonekana katika tarakimu za Umoja wa Mataifa kwamba nchi hiyo imekwenda chini, ni suluhisho jumla la kisiasa, suluhisho ambalo litatilia maanani ukubwa ulio wazi ambao mzozo huo wa Somalia umechukuwa katika eneo hilo.

Bila ya shaka, wanasiasa wa Kisomali na wababe wa kivita wa nchi hiyo ambao tangu mwaka 1991 wameirejesha nyuma nchi hiyo katika enzi za kale wanabeba dhamana. Hasa Rais Abdullahi Yussuf, mbabe wa kivita asiyekuwa na sifa nzuri, mtu ambaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linamn'gan'gania, bila ya msingi.

Pia jamii ya kimataifa inabeba lawama. Tangu ile Operesheni ilioongozwa na Marekani, iloshindwa mwanzoni mwa miaka ya tisini, na kupewa jina la Kurejesha Matumaini katika Somalia, jamii ya kimataifa, chini ya uongozi wa Marekani wanaosumbuliwa bado na kushindwa kwao, jamii hiyo ya kimataifa haijatunga tena siasa madhubuti kuelekea Somalia au kuelekea Pembe ya Afrika. Makosa yaliofanyika, kama vile Marekani kuuunga mkono Muungano wa ajabu wa wababe wa kivita au kivishambulia bila ya kuchaguwa vijiji vya Wasomali, yamefanya itikisike imani ya Wasomali juu ya mfumo wa suluhisho kutoka nchi za Magharibi.

Na zaidi, kuna jambo moja katika mazungumzo haya ya sasa ambalo linaachwa kabisa. Ni meli za uvuvi za Kirussia, Kichina na kutoka Spain ambazo zinavuwa kiholela katika pwani ya Somalia, hivyo kuwapokonya wavuvi wa Kisomali msingi wa kuendesha maisha yao.Pia ule mtindo ulioendelea kwa miaka wa kutupa takataka baharini, kwa njia isiokuwa ya kisheria, kulikoendeshwa na dola la zamani la kikoloni, Italy, sasa madhara yake yanaonekana katika mfumo wa uharamia.

Marekani iliwasilisha mada ya uharamia wa baharini mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ni jambo la kupongezwa, lakini linaponya tu alama za mzozo wa Somalia. Ingekuwa bora kwa Marekani, kama vile ilivofanya Jumuiya ya kimkoa ya nchi za Pembe yaa Afrika, IGAD, kuiwekea wakati wa mwisho serekali ya mpito ya Somalia isiofanya kazi, na kuilazimisha iziingize pande zote za kisiasa katika mwenendo wa kutafuta amani ya nchi hiyo. Mpango wa amani wa karibuni uliofikiwa huko Jibuti, licha ya makosa yake yote, unaweza ukawa ni msingi wa mwenendo wa kutafuta amani.
 • Tarehe 19.12.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GJrH
 • Tarehe 19.12.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GJrH
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com