1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Blinken : Israel haina haki tu bali pia wajibu wa kujilinda

Admin.WagnerD3 Novemba 2023

Wanajeshi wa ardhini wa Israel wameuzingira mji wa Gaza, huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akifanya ziara nchini Israel.

https://p.dw.com/p/4YNt1
Antony Blinken akifanya ziara nchini Israel na kutangaza kuwa nchi hiyo ina haki na wajibu wa kujilinda
Antony Blinken akifanya ziara nchini Israel na kutangaza kuwa nchi hiyo ina haki na wajibu wa kujilindaPicha: Amos Ben Gershom/Israel Gpo/ZUMA Wire/IMAGO

Kabla ya kuwasili kwa Blinken huko Israel, jeshi la nchi hiyo lilisema limekamilisha kuuzingira mji mkubwa zaidi wa Gaza, ikiashiria hatua mpya katika mzozo wa karibu mwezi mzima.

Leo Ijumaa, mashambulizi mapya ya Israel yalitikisa Ukanda wa Gaza, huku  wizara ya afya ya ukanda huo ikiripoti vifo vya watu 15 katika kitongoji cha Zeitun na wengine saba katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia.

Kabla ya kuelekea Israel, Blinken alisema atajaribu kuhakikisha kuwa madhara kwa raia wa Palestina yanapungua, lakini, wakati wa mazungumzo na Rais Isaac Herzog, Blinken alisisitiza msingi wa uungwaji mkono wa Marekani, akiwaambia waandishi wa habari kuwa Israel haina haki tu bali pia wajibu wa kujilinda. Blinken anasema walijadiliana pia na Waziri Mkuu wa Israel kuhusu misaada ya kibinadamu Gaza.

'Tunaamini kwamba kila moja ya juhudi hizi itawezeshwa na kusitishwa kwa mapigano kwa ajili ya misaada ya kibinadamu, kwa mipango ya msingi ambayo inaongeza usalama kwa raia na kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa ufanisi zaidi na endelevu. Hili lilikuwa jambo muhimu la majadiliano leo na viongozi wa Israeli: jinsi gani, lini na wapi hii inaweza kutekelezwa? Ni kazi gani inapaswa kufanyika na ni uelewa gani unapaswa kufikiwa? Sasa tunatambua kwamba hii itachukua muda kufanyika na kuratibu pamoja na washirika wa kimataifa.", alisema Blinken. 

''Mafanikio ya kuvitia sana'' 

Wanajeshi wa Israel wauzingira mji wa mkubwa wa Gaza
Wanajeshi wa Israel wauzingira mji wa mkubwa wa GazaPicha: Israel Defense Forces via AP/ Photo/picture alliance

Blinken amesema pia kwamba njia pekee ya kuhakikisha usalama wa Israel ni kuundwa kwa taifa la Palestina, baada ya kukutana na viongozi wa Israel.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema Israel tayari ilikuwa na mafanikio ya kuvutia sana na wanajeshi zaidi wamefikia viunga vya Mji wa Gaza na wanasonga mbele. Na hakutakuwepo na usitishwaji mapigano pasina kuachiwa huru mateka wa Israel.

Wakati huo huo, Israel ilianza kuwafukuza maelfu ya wafanyakazi wa Kipalestina kurejea Gaza, licha ya mapigano yanayoendelea na mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya raia katika eneo hilo.

Mafuta kupelekwa Gaza ?

Huko Geneva, Umoja wa Mataifa umezindua ombi la msaada wa dharura wa dola bilioni 1.2 kusaidia watu karibu milioni 2.7 wanaokabiliwa na janga la kibinadamu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Huko NewYork , Mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths amesema kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo ya kimataifa ya kuruhusu mafuta kuingia katika ukanda wa Gaza.

Mazungumzo hayo yanafanyika baina ya Umoja wa Mataifa, Israel, Misri na Marekani. Hata hivyo Griffiths alirejelea wito wake wa kuweko na usitishwaji mapigano kwa ajili ya kupelekwa misaada ya kibinadamu.