1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel latangaza kuuzingira kikamilifu Mji wa Gaza

3 Novemba 2023

Msemaji wa jeshi Daniel Hagari amesema jana usiku kuwa wanajeshi wa Israel pia wameharibu vituo vya kijeshi vya kundi la Hamas na miundo mbinu wakati likiingia katika Mji wa Gaza kutokea pande kadhaa

https://p.dw.com/p/4YLZC
Jeshi la Israel katika Gaza
Vikosi vya Israel vimeuzingira kikamilufu mji wa GazaPicha: Israel Defense Forces via AP/ Photo/picture alliance

Jeshi la Israel limetangaza kuuzingira kikamilifu mji wa Gaza. Msemaji wa jeshi Daniel Hagari amesema jana usiku kuwa wanajeshi wa Israel pia wameharibu vituo vya kijeshi vya kundi la Hamas na miundo mbinu wakati likiingia katika Mji wa Gaza kutokea pande kadhaa. Hapo awali, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa Israel ipo katika kilele cha mapambano, na imekuwa na mafanikio makubwa. Tangu wiki iliyopita, Israel imeimarisha mashambulizi ya ardhini kaskazini mwa Gaza kwa kuwalenga wanamgambo wa Hamas waliojaa katika Mji wa Gaza.

Soma pia: Vita vya Israel na Hamas: Idadi ya waliouawa yafikia 9,000

Makombora ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Israel imeendelea kudondosha makombora GazaPicha: Fadel Senna/AFP/Getty Images

Jeshi la Israel lilisema kuwa mafuta yataruhusiwa kuingia Gaza kwa ajili ya hospitali zitakazoishiwa na bidhaa hiyo. Hata hivyo lilisema hilo litafanyika chini ya uangalizi.

Mamia ya maelfu ya raia wa Kipalestina wamenasa katika mapigano hayo, licha ya miito ya mara kwa mara ya Israel kuwataka wahamie kusini mwa Gaza, ambako pia kunapigwa na mashambulizi ya kutokea angani.

Hezbollah yayapiga maeno ya mpakani Israel

Kundi la Hezbollah la Lebanon limesema limeyapiga maeneo 19 ya Israel kwenye mpaka wa nchi hiyo, hatua iliyosababisha shambulizi pana la kulipiza, kwenye mkesha wa hotuba ya kiongozi wa kundi ilo linaloungwa mkono na Iran kuhusu vita vya Israel na Hamas. Shirika la huduma za dharura za matibabu la Israel limesema mfululizo mwingine wa makombora uliwajeruhi watu wawili katika mji wa Israel wa Kiryat Shmona karibu na mpaka na LEBANON.

Mpaka wa Israel na Lebanon umeshuhudia makabiliano ya kila upande, hasa kati jeshi la Israel na mshirika wa Hamas Hezbollah, tangu wanamgambo hao wa Kipalestina walipoishambulia Israel mnamo Oktoba 7 kutokea Ukanda wa Gaza na kuzusha hofu ya mzozo wa kikanda.  

Antony Blinken na Benjamin Netanjahu
Waziri Blinken ataishinikiza Israel kupunguza madhara kwa raia wa Ukanda wa GazaPicha: Jacquelyn Martin/Pool via REUTERS

Kiongozi mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah anatarajiwa kuzungumza Ijumaa kwa mara ya kwanza tangu kuzuka vita kati ya Israel na Hamas.

Blinken aelekea Israel kwa mara nyingine

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marakeni Antony Blinken ameelekea Israel ambako atatafuta hatua mwafaka kutoka kwa Israel za kupunguza madhara kwa raia wa Gaza. Ni ziara yake ya pili ya dharura katika Mashariki ya Kati tangu shambulizi la Hamas ndani ya Israel lilipozusha vita. Blinken ameyasema hayo wakati akianza safari yake, siku moja kabla ya mkutano wake wa karibuni kabisa na Waziri Mkuu Benjamin Nentanyahu. Blinken atakuwa Israel siku nzima leo Ijumaa, na kisha ataelekea Jordan na pengine vituo vingine kabla ya kuelekea Asia katika ziara iliyopangwa hapo kabla.

Soma pia: MSF: Majeruhi zaidi ya 20,000 bado wamekwama Gaza

Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limekemea ukosefu wa uhakikisho wa usalama kwa ajili ya kupelekwa misaada ya kibinaadamu katika Ukanda wa Gaza. WHO imesema haiwezekani kabisa kuingiza msaada wa matibabu kwa hospitali za eneo hilo. Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema WHO itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa watu wote Gaza wanapata huduma za afya na za kiutu zinazohitajika kwa dharura. Wizara ya afya ya serikali ya Hamas katika Ukanda wa Gaza inasema Zaidi ya watu 9,000 wameuawa tangu kuzuka vita na Israel, wengi wao wanawake na Watoto. Tedros amesema hawana tena maneno ya kuelezea ukatili unaoshuhudiwa Gaza.

afp, ap, reuters, dpa