BERLIN: Sarkozy akutana na Merkel leo | Habari za Ulimwengu | DW | 10.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BERLIN: Sarkozy akutana na Merkel leo

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, leo atakutana na kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, mjini Berlin.

Mazungumzo kati ya viongozi hao, ambayo si rasmi, yatatuwama juu ya juhudi za jimbo la Kosovo kutaka kuwa huru kutoka kwa Serbia na matatizo yanayoyakabili masoko ya fedha.

Viongozi hao watajadili njia za kupata ufanisi katika mazungumzo kuhusu hatima ya jimbo la Kosovo na vipi kuhakikisha Umoja wa Ulaya unabakia kuungana licha ya tofauti za kimawazo kati ya nchi wanachama.

Kansela Merkel na rais Sarkozy ambao wamekuwa wakifanya juhudi kuwa na uhusiano wa karibu na Marekani, watajaribu kuzitatua tofauti zao wakati watakapokutana katika kasri lililo kaskazini mwa mji mkuu Berlin, kwenye mkutano utakaohudhuriwa pia na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani na Ufaransa.

Viongozi hao wana msimamo mmoja kuhusu swala la Kosovo huku kukiwa na mgawanyiko miongoni mwa wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya kuhusu kuutambua uhuru wa Kosovo iwapo jimbo hilo litatangaza uhuru wake kutoka kwa Serbia.

Huku Ufaransa ikiwa tayari kujiunga na Uingereza na Marekani kuutambua uhuru wa Kosovo, Ujerumani bado inasita kutangaza msimamo wake ikiwa na matumaini ya kufikia makubaliano.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com