1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Kansela Schröder aalikwa futari Uturuki.

12 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CESi

Kansela wa Ujerumani anayeondoka madarakani Gerhard Schröder anaonekana kuwa ameondoa uwezekano wa kukubali nafasi ya uwaziri katika serikali ya mseto chini ya kiongozi wa chama cha Christian Democratic Union CDU Angela Merkel.

Akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara mjini Berlin , Schröder amesema atafanyakazi kuhakikisha kuwa mazungumzo yanayokuja juu ya muungano kati ya chama cha CDU na kile anachokiongoza cha Social Democrats yanafanikiwa.

Haya amesema kuwa bado ni majukumu yake , hata kama hatakuwa mmoja kati ya viongozi katika serikali ijayo.

Siku ya Jumatatu vyama vya CDU na SPD vilitangaza kimsingi kuunda kile kinachofahamika kuwa ni muungano mkuu katika serikali ya mseto , na Merkel akiwa ni kansela.

Merkel na Schröder wamedai kuwa wamepewa uwezo na wapigakura kuweza kuiongoza serikali ya nchi hiyo, kufuatia uchaguzi wa mwezi uliopita , ambapo chama cha CDU kimeshinda viti vinne zaidi ya SPD.

Wakati huo huo kansela Gerhard Schröder anakwenda Uturuki leo kwa ziara fupi mjini Istanbul.

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemualika Schröder kula nae futari hii leo katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

Lakini pamoja na hayo Bwana Erdogan anataka kutoa shukurani zake kwa serikali ya Bwana Schröder kwa msaada wake katika kuisogeza Uturuki karibu na umoja wa Ulaya, kabla ya kansela huyo wa Ujerumani kuondoka madarakani.