1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Israel iwajibishwe kwa uhalifu wa kivita huko Gaza

5 Aprili 2024

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuitaka Israel kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita na uwezekano wa uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4eSfn
Gevena I Mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Wajumbe wakisikiliza tamko la Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na hali ya haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina wakati akiwasilisha ripoti yake ya mwisho mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.Picha: Fabrice Coffrini/AFP

Jumla ya nchi 28 zimepiga kura ya ndio huku 13 zikijizuia kupiga kura na nyingine sita zikipinga azimio hilo, zikiwemo Marekani na Ujerumani. Kupitishwa kwa azimio hilo kulipokelewa kwa shangwe na baadhi ya wawakilishi wa Baraza hilo.

Hii mara ya kwanza kwa baraza kuu la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kuchukua msimamo juu ya vita vya umwagaji damu kuwahi kushuhudiwa katika eneo la  Palestina lililozingirwa.  

Azimio hilo limesisitiza haja ya kuhakikisha uwajibikaji kwa vitendo vyote vya ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu. Pia ilisisitiza "wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukwaji wa haki na ukiukwaji mkubwa wa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Pia azimio hilo linatoa wito kwa nchi husika kusitisha uuzaji, uhamisho na upelekaji wa silaha na vifaa vingine vya kijeshi kwa Israel, na kwamba hilo linahitajika miongoni mwa mambo mengine ili kuzuia ukiukaji zaidi wa haki na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Geneva | Kura ya azimio kuhusu mzozo wa Israel na Hamas huko Gaza
Matokeo ya kura ya azimio kuhusu mzozo wa Israel na Hamas huko Gaza: Geneva 05.04.2024Picha: Salvatore di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Azimio hilo limesisitiza kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ilitoa uamuzi mwezi Januari kwamba kuna hatari inayowezekana ya kutokea mauaji ya kimbari huko Gaza.

Soma pia: Uingereza yashinikizwa kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel

Azimio hilo lililopitishwa leo, liliwasilishwa na Pakistan kwa niaba ya nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) isipokuwa Albania, inatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuwepo usaidizi wa dharura  huko Gaza. Bilal Ahmad, Mwakilishi wa kudumu wa  Pakistan katika Umoja wa Mataifa amesema:

" Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, mamlaka inayokalia kwa mabavu imeandika ukurasa mpya na wa kutisha katika mkasa huu wa miaka 75 wa watu wa Palestina. Rasimu ya azimio hili imeandaliwa kwa lengo la kujibu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoshuhudiwa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa, haswa katika Ukanda wa Gaza."

Meirav Eilon Shahar, mwakilishi wa kudumu wa Israel Umoja wa Mataifa huko Geneva, amelishutumu Baraza hilo na kusema limewatelekeza  watu wa Israel na kutetea kundi la Hamas kwa muda mrefu.

Israel kuongeza uwasilishwaji wa misaada Gaza

Benjamin Netanjahu na Rais wa Marekani Joe Biden
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) akiwa na Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Michael Gottschalk/picture alliance/photothek

Israel imesema leo kuwa itachukua hatua za kuongeza mtiririko wa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kufungua tena kivuko muhimu cha mpakani kaskazini mwa ukanda wa Gaza. Hata hivyo, tangazo hilo halikufafanua juu ya idadi au aina ya vitu vitakavyowasilishwa eneo hilo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu  imetangaza mipango hiyo

saa chache baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na Netanyahu na kumueleza kuwa katika siku zijazo msaada wa Washington kwa Tel-Aviv utategemea na hatua za Israel katika kuwalinda raia pamoja na  wafanyakazi wa mashirika ya misaada.

Licha ya tofauti zao, utawala wa Biden umeendelea kuipatia Israel misaada muhimu ya kijeshi na kidiplomasia katika vita hivi kati ya Israel na kundi la Hamas vilivyodumu kwa miezi sita na ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 33,000, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya huko Gaza inayodhibitiwa na kundi la Hamas.

Aidha rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema Israel inapaswa kusitisha operesheni yake huko Gaza kwa kuwa imeshindwa kabisa linapokuja suala la vita vya kimkakati vya mawasiliano kutokana na picha za kila siku zinazoonyesha jengo la ghorofa likiteketea katika Ukanda wa Gaza.

(Vyanzo: Mashirika)