Asasi za kiraia Tanzania zakabiliwa na ukata mkubwa
22 Aprili 2026
Asasi nyingi zisizo za kiserikali (NGOs) nchini Tanzania zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha, hali iliyosababisha takriban asasi 81 kufunga ofisi zao, huku nyingine kadhaa zikiwa katika hatari ya kusitisha shughuli zake. Kupungua kwa ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo kumetajwa kuwa chanzo kikuu cha hali hiyo.
Taarifa hiyo imebainika kufuatia utafiti mdogo uliofanywa na , ambao pia unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa rasilimali za kuendesha shughuli zake. Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa wafadhili wakubwa wamepunguza au kusitisha kabisa ufadhili wao kwa asasi mbalimbali za kiraia nchini.
Miongoni mwa wafadhili waliopunguza au kusitisha ufadhili ni United States Agency for International Development, ambayo ilisimamisha msaada wake tangu mwaka 2023. Aidha, serikali ya Sweden kupitia Swedish International Development Cooperation Agency ilitangaza mwaka 2024 kuwa haitaendelea tena kufadhili miradi ya asasi hizo nchini Tanzania.
Wafadhili wengine kutoka barani Ulaya, wakiwemo wale kutoka Ujerumani, nao wako katika mwelekeo wa kupunguza au kusitisha misaada yao. Sababu kuu inayotajwa ni mabadiliko ya vipaumbele vya kimataifa, ambapo rasilimali nyingi zimeelekezwa katika migogoro mingine mikubwa kama vita vya Ukraine.
Kaimu Mratibu wa THRDC Zanzibar, Shadida Omar, anasema hali hiyo tayari imeanza kuathiri utoaji wa huduma muhimu kwa jamii.
Athari kwa huduma na ajira za wananchi
Kwa mujibu wa maelezo yake, kufungwa kwa ofisi za wafadhili na kupungua kwa fedha kumesababisha kupungua kwa huduma katika sekta muhimu kama haki za binadamu, afya na elimu. Aidha, ajira nyingi zimepotea na sauti ya wananchi imeanza kudhoofika.
"Ni muhimu sasa asasi za kiraia kubadili mikakati kwa kutafuta vyanzo vya ndani, kuimarisha uwazi na kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine,” anasisitiza.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, baadhi ya asasi zimeanza kutafuta mbinu mbadala za kujitegemea kifedha ili kuhakikisha huduma kwa jamii zinaendelea. Miongoni mwao ni Mwemvuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar (ANGOZA) pamoja na mashirika yanayojihusisha na maendeleo ya vijana.
Afisa Programu wa ZAFAYCO, Aziza Jaffery, anasema shirika lake lilipokea zuio la ufadhili kutoka USAID mapema mwaka 2025, hali iliyoathiri mradi uliolenga kuwasaidia takriban vijana 3,000 kushiriki katika shughuli za kidemokrasia.
Mikakati mipya ya kujitegemea
Kwa upande wake, Maalim Hassan Khamis wa ANGOZA anaeleza kuwa asasi zimeanza kubuni njia mbadala za kukabiliana na hali hiyo.
Anasema baadhi ya mikakati inayotumika ni pamoja na ushirikiano kati ya asasi katika kugharamia shughuli mbalimbali, kuchangisha ada za wanachama, pamoja na kuanzisha miradi ya kijamii inayoweza kuzalisha kipato.
"Tunajaribu kushirikiana kwa karibu zaidi, kugawana gharama za shughuli na pia kuangalia uwezekano wa kuanzisha miradi ya ndani ili kupata fedha za kuendesha programu zetu,” anaeleza.
Kwa ujumla, licha ya changamoto hizi, asasi za kiraia zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii nchini Tanzania, zikitoa mchango mkubwa katika sekta za afya, elimu, haki za binadamu na uchumi.
Hata hivyo, uhaba wa rasilimali fedha unaendelea kuwa tishio kwa uendelevu wa shughuli zao, hali inayosisitiza umuhimu wa kubuni mikakati mipya ya ndani na kuimarisha ushirikiano wa wadau mbalimbali.