HRW: Tanzania acheni vitisho kwa asasi za kiraia | Matukio ya Afrika | DW | 06.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

HRW: Tanzania acheni vitisho kwa asasi za kiraia

Mashirika 18 yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje ya Tanzania yameitaka serikali ya nchi hiyo kuacha lugha za chuki dhidi ya asasi za kiraia pamoja na vitisho vinavyolenga kuzuia utekelezaji wa kazi za asasi hizo.

Serikali ya Tanzania hivi karibuni imetoa kauli zinazolenga asasi zinazowasaidia wanafunzi wa kike waliopata ujauzito kuweza kuendelea na masomo na mashirika yanayotetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja. 

Taarifa iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, inasema rais wa Tanzania na maafisa wa juu wanapaswa kuweka mkazo wa namna gani ya kujenga nchi kwa kumsaidia kila mmoja kumaliza elimu yake na kukomesha ubaguzi.

Kauli za hivi karibuni za maafisa wa serikali zinaweza kuwa na athari mbaya kwa mashirika yaliyoathirika, imesema taarifa hiyo. Mnamo Juni 22, Rais John Magufuli alinukuliwa akisema kuwa wakati wa utawala wake hakuna mwanafunzi mjamzito atakayeruhusiwa kurudi shuleni, na kuongeza kwamba wanafunzi hao wanaweza kusoma katika vyuo vya mafunzo ya ufundi au wawe wajasiriamali, lakini hawapaswi kupewa nafasi ya kurudi katika shule za umma. Katika hotuba hiyohiyo pia rais alitoa kauli juu ya mahusiano ya jinsia moja.

Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba naye alikaririwa akitishia kufuta usajili wa mashirika yanayopinga kauli ya rais ya kupiga marufuku wanafunzi waliopata mimba kurejea mashuleni ama yale yanayotetea haki za mashoga na wasagaji. Serikali inakadiria kuwa wasichana 30 kati ya kila 100 waliacha shule kutokana na ujauzito mwaka 2015.

Tansania John Magufuli (Getty Images/AFP/D. Hayduk)

Rais wa Tanzania John Magufuli

Kauli za hivi karibuni za rais Magufuli na waziri wake Nchemba zinakinzana na juhudi za muda mrefu zilizofanywa na wizara ya elimu, sayansi na teknolojia na asasi za kiraia za kuanzisha miongozo ya kuwapokea upya wanafunzi waliopata mimba na kuhakikisha wanaendelea na masomo  baada ya kujifungua. Chama tawala nchini humo chama cha mapinduzi CCM, katika ilani yake ya mwaka 2015, kiliahidi kuwa kitahakikisha wanafunzi hao wanaendelea na masomo baada ya kujifungua.

Mwaka 2015, kamati maalumu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu, ilielezea wasiwasi wa kukosekana kwa sheria inayozuia kufukuzwa kwa wasichana shuleni kwasababu ya ujauzito. Kamati hiyo iliitaka serikali ya Tanzania kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha wasichana hao wanaandikishwa mashuleni, kuunga mkono na kuwasaidia wasichana kuendelea na elimu yao katika shule za umma.

Kauli za serikali ya Tanzania zinakwenda kinyume na majukumu ya haki za binadamu ya ndani na nje. Hii ni pamoja na jukumu la kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata elimu ya msingi na sekondari, bila ya ubaguzi pamoja na kuhakikisha kwamba wale waliopata mimba wanarudi shule na kumaliza elimu yao. Haki ya kampeni ya usawa kwa wote bila ya kujali mwelekeo na utambulisho wa kijinsia, kuwa nayo inazingatiwa.

Taarifa hiyo imehitimisha kwa kusema kuwa asasi zote za kiraia zinapaswa kuruhusiwa kutekeleza shughuli zake bila ya hofu ya kufutwa kwa tafiti zake, uhamasishaji, programu na huduma wanazotoa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/HRW

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com