Angela Merkel afunika matatizo badala ya kuyatatua. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.12.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Angela Merkel afunika matatizo badala ya kuyatatua.

kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakabiliwa na matatizo makubwa hapo baadaye iwapo hatafafanua anasimamia kitu gami pamoja na chama chake cha CDU, hususan katika uchaguzi mkuu ujao.

Kansela Angela Merkel huenda anahifadhi matatizo kwa kuweka kando maamuzi magumu ya kisera ili kuweza kukielekeza chama chake katika nafasi ya kati ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2009.

Kwa hivi sasa , Merkel anapata alama za juu kabisa katika kura ya maoni akiwa kama kansela maafuru sana tangu baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Kutokana na ukweli kwamba huenda ukuaji wa uchumi unaweza kupungua kasi ikiwa ni pamoja na mtazamo wa kimapambano zaidi kutoka kwa washirika katika serikali ya mseto chama cha Social Democratic SPD, inaweza kuchangia katika mwaka wa matatizo zaidi wa 2008 wakati kutakuwa na uchaguzi katika majimbo manne nchini Ujerumani.

Huu utakuwa mtihani kwa umaarufu wa Merkel pamoja na chama chake cha Christian Democratic CDU kabla ya uchaguzi mkuu hapo mwaka 2009 na wengi wa wadadisi wa masuala ya kisiasa wanatumaini kuwa utayarishaji wa sera unaweza kutolewa mhanga zaidi na zaidi kwa minajili ya kupata kura.

Mambo yanaonekana kuwa shwari hivi sasa kwa Merkel lakini kuna ishara kuwa hali haitabaki kuwa hivyo, amesema Frank Decker, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika chuo kikuu cha Bonn.

Hali ya kiuchumi inaweza kabisa kuporomoka, chama cha SPD huenda kisibakie kuwa dhaifu kwa muda mrefu, na zaidi ya yote bibi Merkel anahitaji kuhakikisha kuwa kila mmoja anafahamu kile anachopigania.

Merkel aliongeza udhibiti wake katika mkutano wa chama chake cha Christian Democratic wiki iliyopita na kiongozi huyo muumini wa madhehebu ya Kiprotestant alikuwa anaogelea katika dakika zaidi ya nane za kushangiliwa kutoka kwa wajumbe wa chama chake ambacho kinawafuasi wengi wa madhehebu ya Kikatoliki, na ambacho viongozi wake wengi wa ngazi za juu ni wanaume.

Amekuwa kama Simba , amesema mshauri mmoja wa masuala ya kisiasa mwenye makao yake makuu mjini Berlin Richard Schuetze. Anadhibiti sifa zake na anaheshimika na kuogopwa na viongozi wa juu wa chama chake.

Lakini wakati udhibiti wake katika CDU unauhakika , anajikuta katika hali ya kushindwa kujenga mwelekeo katika muungano unaounda serikali na chama cha SPD, ambacho kimejisogeza upande wa shoto ili kuweza kupata kura za waungaji wake wa mkono wa asili.

Wakosoaji wanamshutumu Merkel kwa kushindwa kuchukua nafasi ya uongozi na kuepuka maamuzi magumu ya sera ambazo zinapaswa kutatuliwa kabla ya chama chake kutayarisha ilani ya uchaguzi wa mwaka 2009.

Mkutano huu uliomalizika ulikuwa unafunika zaidi tofauti ndani ya chama cha CDU badala ya kuzitatua na hili linaweza kuwa tatizo katika uchaguzi mkuu ujao iwapo haitakuwa wazi kuwa Merkel na CDU wanasimamia kitu gani hasa, amesema Decker.

Wajerumani wengi wanatarajia miaka miwili ya kampeni miongoni mwa washirika wa muungano wa serikali wakikubaliana katika mambo machache na kulumbana juu ya sera kama kiwango cha chini cha mshahara , mafao ya matibabu kwa watoto, pamoja na ubinafsishaji wa shirika la reli Deutsche Bahn.

Wataalamu wachache wanatarajia muungano wa serikali kuvunjika kabla ya uchaguzi, kwa kuwa pande zote mbili hazingependa kupoteza madaraka , lakini hakuna mtu anayetarajia kitu kikubwa katika mageuzi pia. Merkel Jumatatu iliyopita alifanya juhudi za kuwavuta wapiga kura wa SPD wanaopendelea msimamo wa kati na kutaka kukionyesha chama cha SPD ambacho ni mshirika katika serikali ya muungano kuwa inazuwia mageuzi. Kwa kudai kuwa katika mrengo wa kati kisiasa , dhana isiyo na ufafanuzi yakinifu ambayo inaazma ya kuwavuta wanaviwanda wenye mtazamo wa kati pamoja na wale ambao wanaupendelea mtazamo wa SPD wa taifa lenye kuwapa mafao raia zake, bibi Merkel anajihatarisha kwa kuwatenga baadhi ya watu katika chama chake, amesema Schuetze. Upande wa kulia kidogo, na kidogo upande wa shoto lakini wakati wote kati kwa kati? Katika muda mrefu hali hiyo inamafanikio madogo. Yule anayesema kila kitu mwishowe hasemi chochote, limeandika gazeti linalouzwa sana nchini Ujerumani la Bild.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com