Afrika ya Kati yaenda uchaguzini | Matukio ya Afrika | DW | 21.01.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Afrika ya Kati yaenda uchaguzini

Baada ya uchaguzi kuakhirishwa kwa mwaka mzima, hatimaye wapiga katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanateremka vituoni kesho Jumapili (23 Januari 2011) kuchagua rais na wabunge wao, licha ya uasi wa Kaskazini kuendelea

Rais François Bozizé wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Rais François Bozizé wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Gharama za uchaguzi wa Bunge na Rais unaofanyika kesho kwenye Jamhuri hii ya Afrika ya Kati, si changamoto pekee kwa nchi hii ambayo imeshuhudia miaka mingi ya uasi ulioikwamisha kimaendeleo. Uchaguzi huu ulishawahi kuakhrishwa mara tatu huko nyuma, kwa sababu za ukosefu wa usalama.

"Matatizo ya kiusalama yako kote Kaskazini na Kusini ya nchi, ambako bado kuna makundi ya waasi na pia majangili wanaovamia magari na kuwaibia wasafiri. Robo moja wa raia wako ukimbizini. Kuna kiasi ya wakimbizi 100,000 wa Afrika ya Kati nchini Chad na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo." Anasema mkuu wa kitengo cha Afrika ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Peter Weinstabel.

Lakini Jumapili ya kesho, raia wa Jamhuri ya Kati watakwenda kufanya maamuzi yao kupitia kisanduku cha kura. Kiasi ya vituo 4,500 vitawapokea wapiga kura milioni mbili kupaza sauti zao, jambo ambalo tayari limezusha hamasa kubwa mjini Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo.

Ni Patasse na Bozize

Mgombea urais, Ange-Felix Patasse

Mgombea urais, Ange-Felix Patasse

Miongoni mwa wagombea wanaotarajiwa kunyang'anyia kiti cha urais, ni rais wa zamani Ange-Felix Patasse na rais wa sasa, Francois Bozize. Bozize aliingia madarakani kwa kumpindua Patasse hapo mwaka 2003, lakini miaka miwili baadaye akajihalalisha kwa kushinda uchaguzi.

Kufanyika kwa uchaguzi huu katika mazingira ya haki na huru ndiko kutakakoamua mwenendo wa eneo la Kaskazini la nchi hiyo, ambalo hadi sasa serikali ya Bangui haijakuwa na udhibiti nalo.

Kwa miaka miwili mfululizo, kumekuwapo na juhudi za kutafuta amani katika eneo hilo, lakini kila mara zimekuwa zikikumbana na vikwazo, kikiwemo kile cha baadhi ya makundi ya waasi kukataa kuzungumza na serikali.

Mkataba wa amani na waasi

Ni hivi karibuni tu, wakati uchaguzi huu ukikaribia, ndipo Rais Bozize alipoweza kutiliana saini na makundi ya waasi, jambo ambalo mtaalamu kutoka Shirika la International Crisis Group, Ned Dalby, anaona kuwa linatia moyo.

"Hasa katika wakati huu ambapo rais amefanya makubaliano na viongozi wa makundi ya waasi kwamba uchaguzi lazima ufanyike bila ya kuchafuliwa. Inawezekana kundi kama la CPJP likajaribu kuliharibu zoezi hili, lakini naamini kuwa wapiga kura nchini kote watasonga mbele kufanya uchaguzi." Anasema Dalby.

Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wameweka matarajio yao makubwa kwa uchaguzi huu wa kesho, kwamba utaimaliza miaka kadhaa ya uasi na kwamba utawajengea msingi mzuri wa kujikwamua na matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na kukosekana utulivu wa kisiasa.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi hii hivi sasa imo katika orodha ya nchi kumi masikini kabisa duniani. Kwa hivyo yeyote atakayetangazwa rais, mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, atajikuta na kibarua kigumu cha kumaliza uasi na kuimarisha usalama, kabla ya kuanza kufufua uchumi. Na hadi kuifikia amani ya kweli, bado pana safari ndefu ya kwenda.

Mwandishi: Dirke Köpp/ZPR/Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman