1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini Tanzania na Urusi zinakaribiana zaidi sasa?

4 Juni 2026

Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imeibua maswali kuhusu mustakabali wa diplomasia ya Tanzania, wakati Moscow ikitafuta washirika wapya na Dar es Salaam ikikabiliwa na shinikizo kutoka Magharibi.

https://p.dw.com/p/5EqRf
Urusi Moscow 2026 | Vladimir Putin na Samia Suluhu Hassan katika hafla ya mapokezi ndani ya Kremlin
Rais wa Urusi Vladimir Putin, kulia, na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakipeana mkono wakati wa hafla ya mapokezi katika Jumba Kuu la Kremlin mjini Moscow, Urusi, Jumatano, Juni 3, 2026Picha: Ramil Sitdikov/AP Photo/picture alliance

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anafanya ziara ya siku tatu nchini Urusi katika kile ambacho pande zote mbili zinakiita hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Dar es Salaam na Moscow. Lakini nyuma ya mikutano ya kidiplomasia, mikataba ya biashara na maneno ya urafiki, kuna maswali mapana zaidi kuhusu siasa za kimataifa na mwelekeo wa sera ya nje ya Tanzania.

Katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin mjini Moscow, Samia alielezea safari hiyo kuwa ya kihistoria. Putin naye alisisitiza kuwa Tanzania na Urusi zinatimiza miaka 65 ya uhusiano wa kidiplomasia mwaka huu na akaeleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa Samia kuichagua Urusi kwa ziara yake ya kwanza rasmi ya kiserikali baada ya kuapishwa.

Lakini umuhimu wa ziara hiyo hauko tu katika historia. Inakuja wakati Urusi ikijaribu kuimarisha nafasi yake barani Afrika kufuatia miaka kadhaa ya vikwazo na kutengwa na mataifa mengi ya Magharibi kutokana na vita vya Ukraine. Moscow imekuwa ikitafuta masoko mapya, washirika wapya wa kisiasa na ushawishi mkubwa katika kile kinachoitwa "Ulimwengu wa Tatu".

Kwa upande mwingine, Tanzania imejikuta ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya na mashirika ya haki za binadamu kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Marekani imetangaza mapitio ya baadhi ya vipengele vya uhusiano wake na Tanzania huku baadhi ya maafisa wa Tanzania wakikumbwa na hatua za vikwazo.

Katika mazingira hayo, wachambuzi wengi wanaona ziara ya Samia Moscow kama ishara kwamba Tanzania inapanua wigo wa ushirikiano wake wa kimataifa ili kuepuka kutegemea upande mmoja pekee.

Rais Samia afanya mazungumzo na Rais Putin

Je, Tanzania inanufaika nini?

Kwa mtazamo wa kiuchumi, Tanzania ina sababu kadhaa za kutafuta ushirikiano mkubwa zaidi na Urusi. Biashara kati ya nchi hizo mbili imekuwa ikiongezeka na kufikia zaidi ya dola milioni 300 kwa mwaka, huku viongozi wa pande zote wakisema kiwango hicho bado kiko chini ya uwezo halisi wa nchi hizo mbili.

Sekta zinazotajwa kuwa na fursa kubwa ni pamoja na madini, nishati, kilimo, usafiri wa anga, elimu, sayansi na teknolojia. Mradi wa urani wa Mkuju River unaoendeshwa na kampuni ya Rosatom ya Urusi bado unaonekana kuwa moja ya alama kuu za ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Aidha, mipango ya kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za Shirika la Ndege la Tanzania, ATCL, kati ya Dar es Salaam na Moscow pamoja na kuanzishwa kwa Baraza la Biashara la Tanzania na Urusi vinaonyesha kwamba pande zote zinataka kuhamisha mahusiano yao kutoka kwenye historia na kuyaelekeza zaidi kwenye biashara na uwekezaji.

Samia pia anatarajiwa kutumia Kongamano la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg kuitangaza Tanzania kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali. Serikali ya Tanzania inaona jukwaa hilo kama sehemu ya mkakati wake wa diplomasia ya uchumi unaolenga kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kwamba Urusi si miongoni mwa wawekezaji wakubwa zaidi nchini Tanzania wala si chanzo kikuu cha misaada ya maendeleo kama ilivyo kwa Marekani, Umoja wa Ulaya au taasisi za fedha za kimataifa. Hivyo mafanikio ya ziara hiyo yatapimwa zaidi kwa mikataba na uwekezaji halisi utakaozaliwa baada ya mazungumzo hayo.

Urusi Moscow 2026 | Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akishiriki hafla ya kuweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana karibu na Kremlin
Ziara ya Rais Samia nchini Urusi imekuja wakati uhusiano wake na mataifa ya Magharibi ukiwa umeyumba kufuatia matukio ya uchaguzi mkuu wa 2025Picha: Ramil Sitdikov/REUTERS

Urusi inanufaika nini?

Kwa Moscow, ziara ya Samia ina thamani kubwa ya kisiasa kuliko kiuchumi. Tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, Kremlin imekuwa ikijaribu kuonyesha kwamba haijatengwa kimataifa na kwamba bado ina washirika katika Afrika, Asia na Amerika Kusini.

Kwa hiyo, kupokea rais wa nchi yenye ushawishi Afrika Mashariki kama Tanzania ni ushindi wa kidiplomasia kwa Putin. Zaidi ya hayo, Tanzania imekuwa ikifuata sera ya kutofungamana na upande wowote katika migogoro mikubwa ya kimataifa, jambo ambalo Moscow huliona kuwa nafasi ya kuendeleza ushirikiano wake na Dar es Salaam.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikijenga mahusiano yake kwa misingi ya kutofungamana na kambi yoyote, sera iliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere. Katika mtazamo huo, ziara ya Samia inaweza kuonekana si kama kuhamia upande wa Urusi, bali kama mwendelezo wa sera ya kushirikiana na pande zote kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Swali kubwa litakalobaki baada ya ziara hii ni kama Tanzania itaweza kutumia mahusiano yake na Urusi kupata manufaa ya kiuchumi bila kuathiri uhusiano wake na washirika wa jadi wa Magharibi. Hilo ndilo litakaloamua ikiwa safari ya Samia Moscow itakumbukwa kama tukio la kawaida la kidiplomasia au mwanzo wa sura mpya katika sera ya nje ya Tanzania.