Ziara ya Papa Afrika, yagubikwa na matamshi makali ya Trump
13 Aprili 2026
Papa Leo atakuwa kiongozi wa kwanza wa juu wa kikatoliki kuzuru nchi ya kiislamu ya Algeria, anakotarajiwa kutoa ujumbe wa mshikamano kati ya waislamu na wakristo, hii ikiwa ni kulingana na Askofu Mkuu wa Algeria Jean-Paul Vesco. Lakini saa chache kabla ya kutoka Roma kuanza safari yake hiyo, Papa akalengwa kwa matashi makali kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Trump alisema yeye sio mfuasi mkubwa wa kiongozi huyo wa kanisa katoliki, aliyesema anacheza na nchi ambayo ni hatari inayotaka kumiliki silaha za nyuklia.
"Hatutompendelea papa anayesema, ni sawa kuwa na silaha za nyuklia. Hatumtaki papa anayesema ni sawa kuwa na uhalifu katika miji yetu. Sipendi. Mimi sio shabiki mkubwa wa Papa Leo. Ni mtu asiyeamini kuhusu kukomesha uhalifu."
Trump alisema makadinali walimchagua Papa Leo aliyemuita, Kiongozi dhaifu asiyefaa katika masuala ya sera za kigeni, kuchukua nafasi hiyo mwezi Mei mwaka 2025, kwasababu tu yeye ni mmarekani na walitaka kuwa na mahusiano na Washington. Baada ya kumkosoa Papa leo, Trump alituma picha yake katika mtandao wake wa Truth Social akiijvalisha kama yesu kristo na kufanya mzaha wa kuwaponya wagonjwa.
Papa asema hauogopi utawala wa Trump
Hata hivyo Papa Leo amemjibu Trump akisema Vatican itaendelea kuhimiza amani na maridhiano kama inavyohimizwa kidini, huku akisema kamwe hauogopi utawala wa Trump.
Papa Leo aliwahi kukosoa vitisho vya Trump kwa watu wa Iran kwamba ataisambaratisha nchi hiyo na kuirejsha katika enzi za kale, akisema vitisho hivyo havikubaliki, lakini hakumtaja jina moja kwa moja Trump. Amewahi pia kukosoa namna serikali ya Trump inavyoshughulikia suala la uhamiaji akisema juhudi zinazochukuliwa sio za kiutu.
Licha ya hayo kile kinachoonekana kama kumuunga mkono Papa leo, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, anayetokea chama cha siasa kali na aliye rafiki wa Donald Trump alitoa taarifa leo asubuhi akimtakia ziara njema Papa Leo XIV, akisema anatumai ziara yake itakuwa na suluhu ya amani ndani na nje ya mataifa anayoyatembelea na kuwapa matumaini na kuwafariji jamii ya wakristo atakayokutana nayo katika ziara hiyo.
Papa Leo abeba ujumbe wa mshikamano Algiers
Ziara ya Papa Leo iliyoanza hii leo Aprili 13 hadi Aprili 23, 2026 itamfikisha Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea. Atakapofika Algiers Algeria, atakutana na rais Abdelmadjid Tebboune, atazungumza na wanadiplomasia huko na kutoa heshima yake kwa waathiriwa wa vita vya Algeria vya kupigania uhuru wao kutoka kwa Ufaransa vilivyoanza mwaka 1954-1962.
Papa pia atatembelea nyumbani kwa mtakatifu Agostino kutokana na papa mwenyewe kutokea shirika la waagostino. Atatembelea pia mji wa Kaskazini Mashariki wa Annaba ataongoza misa huko na kutoa ujumbe wa mshikamano kabla ya kuutembelea msikiti wa Algiers.
Katika ziara yake hiyo mashirika matatu ya haki za binaadamu nchini humo yamemtaka Papa leo kujadili na viongozi kuhusu ukandamizaji wa dini za waliowachache. Wamesema licha ya katiba ya Algeria kuruhusu uhuru wa kuzungumza bado dini ya waliowachache zinakandamizwa.