Ziara ya Baba Mtakatifu Brazil | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya Baba Mtakatifu Brazil

Miaka miwili baada ya kuchaguliwa baba mtakatifu, Benedikt wa 16, leo hii aliondoka Roma kwa safari yake ya siku nne nchini Brazil. Karibu nusu ya waumini wote wa kikatoliki wanasemekana wanaishi nchini humo.

Wabrazil wamejitayarisha wa ziara ya Papa

Wabrazil wamejitayarisha wa ziara ya Papa

Safari hii ni kazi ngumu kwa Baba Mtakatifu. Licha ya Brazil kuwa ni ngome ya madhehebu ya kikatoliki, eneo zima la Amerika Kusini linakabiliwa na ongezeko kubwa la watu wanaojitenga na kanisa katoliki. Juu ya hayo kuna mjadala mkali juu ya uzazi wa majira na utoaji mimba. Uamuzi wa jiji la Mexico kuruhusa utoaji mimba hadi wiki ya 12 ya mimba unaonekana kuwa kama ushindi dhidi ya kanisa katoliki.

Tayari kabla ya ndege yake kutua nchini Brazil, Benedikt 16. alizungumza na waandishi wa habari wanaomsindikiza na kuzusha ubishani pale alipoonekana kuunga mkono hoja ya kuwatenganisha na kanisa wanasiasa ambao wanapitisha sheria za kuhahalisha utoaji mimba. Hata hivyo, lakini, msemaji wa Papa baadaye alisema, Baba huyu mtakatifu hakutaka kumtenganisha yeyote. Wakati huo huo mjini Brasilia mamia ya waumini waliandamana dhidi ya utoaji mimba.

Benedikt pia alitaja kuhusu changamoto nyingine ambayo kanisa katoliki linakabiliwa nayo huko Amerika Kusini ni elimu ya dini ya upinzani. Harakati hii imeanzishwa miaka ya sitini kwenye mitaa ya watu maskini. Kutokana na umaskini, njaa na hali mbaya ya uchumi, wanatheolojia walianza kuzungumzia maadili ya kikristo si tu kanisani bali pia kwenye jukwaa la kisiasa. Wakikumbusha msingi wa kikristo kwamba mungu anataka binadamu kuishi salama, wanasema lengo la Mungu haliwezekani kutekelezwa kwa sababu mazingira ya kisiasa na kijamii hayafai.

Baba Mtakatifu, kabla ya kuwasili Amerika Kusini alikiri kuwa masuala ya usawa wa kijamii ni muhimu yatajwe na wachungaji, lakini viongozi wa kanisa wanapaswa kutoingia katika siasa. Mwaka 1986, Kardinal Joseph Ratzinger, ambaye leo ni Baba Mtakatifu Benedikt 16. alimhukumu mmoja wa wanaharakati maarufu zaidi wa elimu hiyo, Bw. Leonard Boff alitakiwa kunyamaza kwa sababu ya maandishi yake juu ya elimu ya dini ya mapindizu. Baada ya Boff kuamua kufunga ndoa alipokonywa vyeo vyake vya kanisa.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na Redio Deutsche Welle, Bw. Boff hakubali elimu ya dini ya mapinduzi kushindwa. Alisema:“Kanisa liliimarisha sheria zake. Lakini ushindi dhidi ya dini ya mapinduzi haujafikiwa. Sababu ni kwamba theolojia hiyo iko mahali pote, kwa ni umaskini na unyonyaji duniani unaendelea.”

Katika maelezo yake ya leo, Papa Benedikt alisema mafundisho ya kanisa kuhusiana na suala hilo hayakulenga kufuta msimamo wa kupigia usawa, lakini lengo ni kuonyesha njia sawa, yaani kutofautisha majukumu ya siasa na majukumu ya kanisa.

Katika ziara yake Brazil, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuongoza misa mbili hadharani, kutembelea kituo cha kuwasaidia vijana wanaokula madawa ya kulevya na kufungua mkutano wa maaskofu wa Amerika Kusini na nchi za Carribian ambao hawajakutana tangu miaka 15 iliyopita. Suala kuu kwenye mkutano wao litakuwa upungufu wa waumini wa kanisa katoliki katika eneo hilo zima.

Papa pia alitaja wasiwasi wake juu ya idadi kuwa ya Wakatoliki wanaojiunga na kanisa kiprotestanti au madhehebu mengine lakini alisema hata hivyo ni ishara kwamba watu wana hamu ya kumuabudu Mungu. Ili kupambana na changamoto hiyo, inabidi kanisa katoliki lijitahidi zaidi, alisema Papa.

 • Tarehe 09.05.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHEZ
 • Tarehe 09.05.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHEZ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com