1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Urusi inakiuka ombi la usitishwaji wa vita

6 Mei 2026

​​​​​​​Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema Urusi imekiuka ombi la Kyiv la kusitisha vita, hii ikiwa ni zaidi ya mara 1,800 ya ukiukwaji wa maamuzi ya upande mmoja ya kusimamisha vita kati ya mataifa hayo jirani.

https://p.dw.com/p/5DNc3
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: SANA/AFP

Moscow awali ilitangaza kusitisha vita kuanzia siku ya Ijumaa ili kupisha maadhimisho ya Siku ya Ushindi Juni 9. 

Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amethibitisha hayo kupitia ukusara wake wa mtandao wa X, akisema Urusi imelikiuka tangazo lake la upande mmoja la kusitisha vita.

Ameongeza kuwa Kyiev hii jioni ya leo itafanya maamuzi ya namna itakavyoendeleza hatua hiyo kwa kuzingatia ripoti za kijeshi na kiintelijensia.

Ukraine ilitangaza kusitisha mapigano kuanzia usiku wa kuamkia Jumatano na kuitolea wito Urusi pia kuungana nao.

Hata hivyo, Moscow hapo kabla ilikwishatangaza azma yake ya kusimamisha vita ambayo ingeanza siku ya Ijumaa ili kupisha maadhimisho ya Siku ya Ushindi Juni 9, ikiwa ni kumbukumbu ya ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya jeshi la Wanazi wa Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha mapema, aliishutumu Moscow kwa kukiuka usitishwaji huo wa mapigano, akisema mashambulizi ya Urusi iliyofyatua droni 108 na makombora matatu yaliendelea kwa usiku mzima, ikiwa ni pamoja na shambulizi la mapema asubuhi kwenye mikoa ya Kharkiv na Zaporizhzhia.

Ameandika kwenye mtandao wa X kwamba, kwa mara nyingine Moscow imepuuza uhalisia na miito ya haki ya kumaliza uhasama, ikisaidiwa na mataifa mengine na mashirika ya kimataifa.

Akaongeza hiyo inaonyesha kwamba Urusi haina mpango na amani na miito yake ya uwongo ya kusitisha mapigano Mei 9 haina uhalisia wowote kwenye diplomasia. Akamalizia kwa kudai kuwa anachojali Rais Vladimir Putin ni gwaride la kijeshi tu na si maisha ya binadamu.

Ujerumani: kanuni za usalama EU ziangaliwe upya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul ametahadharisha kwamba kanuni ya Umoja wa Ulaya inayotaka uamuzi wa pamoja (unanimity) inaiweka jumuiya hiyo katika hatari yanapokuja masuala ya usalama, akitolea mfano Ukraine na kusema kuwa Ujerumani itawasiliana na nchi wanachama ambazo bado zina wasiwasi kuhusu pendekezo la kubadilisha sheria hiyo na kuweka utaratibu wa upigaji kura wa walio wengi. Tayari mataifa 12 yanaunga mkono mabadiliko ya kanuni hiyo hadi sasa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul

Huku hayo yakijiri, Rais Zelenskiy mchana wa leo ametangaza kwamba Hungary imerejesha fedha taslimu na dhahabu ilizozikamata kutoka kwa wafanyakazi wa benki inayomilikiwa na serikali ya Ukraine ya Oschadbank mnamo mwezi Machi, katikati ya mvutano mkali wa kisiasa kati yake na Budapest.

Zelensky amesema kupitia mitandao ya kijamii kwamba hatua hiyo ni muhimu kimahusiano na Hungary na kuipongeza kwa kutumia mbinu za kiistaarabu. 

Kyiv iliishutumu Budapest kwa kuwachukua mateka kwa kuwatia kizuizini wafanyakazi saba wa Oschadbank waliokuwa wakisafiri kupitia Hungary wakiwa na dola milioni 40, yuro milioni 35 na kilo tisa za vipande vya dhahabu ambavyo pia vilikamatwa.