1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aapa Ukraine kuishinda Urusi

Mohammed Khelef
24 Februari 2023

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ameapa kwamba mwaka huu wa 2023 utakuwa mwaka wa ushindi dhidi ya uvamizi wa Urusi, huku Muungano wa Kijeshi wa NATO ukisema dhamira yake ya kuiunga mkono Ukraine iko imara.

https://p.dw.com/p/4NvZv
Ein Jahr Krieg in der Ukraine - Selenskyj in Butscha
Picha: President Of Ukraine/ZUMA Press Wire Service/dpa/picture alliance

Rais Zelensky ametumia hotuba yake ya kukumbuka mwaka mmoja wa uvamizi wa Urusi dhidi ya nchi yake kunadi ujasiri na dhamira ya jeshi la Ukraine kutetea mipaka ya nchi hiyo.

"Siku kama hii mwaka mmoja uliopita kutoka mahala hapa hapa majira ya saa moja asubuhi, niliwahutubia kwa maelezo mafupi. Ilikuwa ya sekunde 67 tu. Ilikuwa na mambo mawili muhimu kabisa kwa wakati huo na sasa. Kwamba Urusi ilianzisha vita dhidi yetu. Na sisi ni madhubuti. Tuko tayari kwa lolote. Tutamshinda kila mtu, kwa sababu sisi ni Ukraine. Hivyo ndivyo ilivyoanza tarehe 24 Februari 2022. Siku refu kabisa maishani mwetu. Siku ngumu kabisa kwenye historia yetu. Tuliamka mapema na tangu hapo hatujalala tena." Alisema rais huyo. 

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waamuru Urusi iondoe vikosi vyake Ukraine
Marekani yawatuhumu mawaziri wa Urusi kwa unyama Ukraine

Akiwa na uso wa huzuni kutokana na mwaka mmoja wa damu, vifo, wakimbizi, na uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu kutokana na mashambulizi ya Urusi, Zelensky aliwaambia raia wa nchi yake kwamba ushindi wa nchi yao kwenye vita hivi, ni jambo la lazima, licha ya kulemewa vibaya na makombora ya adui.

"Hatutakaa kitako hadi wauaji wa Urusi wakabiliane na adhabu wanayostahiki. Adhabu ya Mahakama ya Kimataifa. Hukumu ya Mungu. Hukumu ya wapiganaji wetu, ama ya wote pamoja. Hukumu ipo wazi. Miaka tisa iliyopita, jirani alikuwa mchokozi. Mwaka mmoja uliopita, mchokozi akawa muuaji, mwizi, na gaidi. Hatuna shaka kuwa watawajibishwa. Hatuna shaka kwamba tutashinda." Alisema.

NATO yaahidi kuendelea kuisaidia Ukraine

Wakati mwaka huu mmoja ukitimia tangu Urusi kuivamia Ukraine, washirika wakuu wa Kyiv, Jumuiya ya Kujihami ya NATO walitangaza siku ya Ijumaa (Februari 24) kwamba hautayumba kwenye msimamo wake wa kuliunga mkono taifa hilo na kwamba juhudi za Urusi kuvunja dhamira ya watu wa Ukraine zinashindwa.

Deutschland | Ukrainische Flaggen am Reichstag in Berlin zum 1. Jahrestag der russischen Angriffs auf die Ukraine
Bendera ya Ukraine ikipepea kwenye jengo la bunge la Ujerumani mjini Berlin siku ya tarehe 24 Februari 2023 kukumbuka mwaka mmoja wa uvamizi wa Urusi.Picha: Fabrizio Bensch/REUTERS

"Urusi lazima isitishe mara moja vita vyake haramu ambacyo vinaathiri usambazaji chakula na nishati duniani, na lazima iwajibishwe kwa uhalifu wake wa kivita. Tunaendelea kuunga mkono kisiasa na kiuchumi na tutaendelea kuwasaidia Waukraine wanaojilinda wenyewe kadiri itakavyohitajika." Ilisema taarifa yake iliyotolewa mjini Brussels.

Soma zaidi: Ukraine yaapa kushinda vita dhidi ya Urusi
China yatoa mwito wa kukomeshwa vita vya Ukraine

Mwaka mmoja baada ya kuanza kwa vita hivyo, mataifa ya Magharibi yanakisia kuwa idadi ya vifo na majeruhi ni mamia kwa maelfu, huku athari zake za kiuchumi zinagusa kila pembe ya dunia, iliyogawanyika kuhusiana vita vyenyewe.

Ambapo mataifa ya Magharibi yanaiunga mkono kijeshi, kifedha na kisiasa Ukraine, mataifa makubwa ya upande wa kusini kama vile China, India, Iran na mengineyo yanaishuku hoja ya Wamagharibi kwamba Ukraine inapigania uhuru na demokrasia yake.

Vyanzo: Reuters, AFP, dpa