1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zardari akabiliwa na hatari ya kuanguka

1 Desemba 2009
https://p.dw.com/p/Kmxz
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari.Picha: AP

Utawala wa Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan unaelekea umo hatarini, wakati wito ukizidi kumtaka aachiye madaraka, huku serikali yake ikikabiliwa na uasi wa Wataliban.Kwa upande mwengine kuna shinikizo la Marekani kuitaka Pakistan isaidie kupambana na wapiganaji nchini Afghanistan.

Mvutano wa kisiasa ulimlazimisha Rais Zardari kukabidhi mamlaka ya silaha za kinyuklia za Pakistan kwa Waziri wake mkuu wiki iliopita. Hatua hiyo hata hivyo ni sawa na ishara tu, kwa sababu ni jeshi la Pakistan linalodhibiti silaha za nyuklia.

Lakini hatua hiyo kwa upande mwengine inaashiria upinzani anaokabiliana nao Zardari ambaye umaarufu wake uko katika kiwango cha chini kabisa miongoni mwa raia wa kawaida, na wakati huo huo wito wa kumtaka aondoke madarakani ukizidi.

Mtihani kwa serikali ya kiraia:

Mvutano huo unazusha uwezekano wa serikali nyengine ya kiraia kushindwa kumaliza muda wake kamili katika taifa ambalo limetawaliwa na jeshi kwa muda ambao ni zaidi ya nusu ya historia yake ya miaka 62.

Sera zenye za utata za Zardari-kama vile mpango wa msaada wa Marekani ulioekewa masharti- umewakasirisha tangu wapakistani wa kawaida hadi wanajeshi wenye usemi mkubwa.

Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa, Hasan Askari Rizvi alisema , Zardari hakabiliwi na kitisho cha mapema kama vile kuondolewa madarakani katika muda wa wiki nne au sita sijazo, lakini anakabiliwa na shinikizo kubwa na shutuma kali kwa sababu ya tabia yake siku za nyuma.

Lakini mchambuzi huyo anasema pia , kama atarekebisha muelekeo wake basi rais huyo anaweza akaendelea hadi yatakapozuka matatizo mengine mapya.

Dai la upinzani:

Upande wa upinzani unamtaka Zardari apunguze madaraka makubwa aliyoyarithi kutoka kwa mtangulizi wake Jenerali Pervez Musharraf ambaye ushirikiano wake na Marekani katika kupambana na ugaidi na hatua yake ya kuayaingilia mahakama, hatimae ni mambo yaliochangia katika kuanguka kwake.

Pervez Musharraf
Mtangulizi wa Zardari, Jenerali Pervez Musharraf .Picha: dpa - Report

Msamaha ndiyo uliomfungulia njia Zardari na mkewe Benazir Bhutto kurudi nyumbani kutoka uhamishoni Oktoba 2007. Bibi Bhutto aliuliwa miezi miwili na kitu baadae na kuacha uongozi wa chama kuelekea uchaguzi mkuu Februari 2008 kushikwa na mumewe na baadae kuwa rais pale Musharraf alipojiuzulu mwezi Agosti mwaka jana.

Changamoto kwa Marekani:

Wachambuzi wanasema kuanguka kwa Zardari kutazusha matatizo katika juhudi za Marekani kutafuta uungaji mkono zaidi katika mapambano dhidi ya wataliban nchini Afghanistan. Kushindwa kwa lengo hilo bila shaka pia kutahujumu nafasi ya Urais ya Barack Obama.

Pamoja na matatizo ya ndani ya Pakistan lakini wadadisi wa mambo wanaashiria kuwa kuendelea kubakia madarakani kwa Asif Ali Zardari kama rais wa Pakistan, kutategemea zaidi miongoni mwa mambo mengine, mafanikio ya sera ya Marekani kuelekea Afghanistan, pamoja na mchango wake wa kuisaidia serikali ya Pakistan kupambana na Wataliban ndani ya Pakistan yenyewe.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman/Reuters

Mhariri:Aboubakary Liongo