1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waukraine kudai fidia kwa uharibifu wa vita vya Urusi

Bruce Amani
2 Aprili 2024

Mawaziri na maafisa kutoka nchi kadhaa wamekusanyika Uholanzi kwa mkutano wa kurejesha haki nchini Ukraine, wakati vita vilivyoanzishwa na uvamizi wa Urusi vikiendelea kurindima ikiwa ni katika mwaka wake wa tatu

https://p.dw.com/p/4eL0X
Mkutano wa kurejesha haki Ukraine
Mfumo wa Waukraine kudai fidia kwa uharibifu wa vita vya Urusi umezinduliwa rasmi katika kongamano la The HaguePicha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Miongoni mwa wazungumzaji katika kongamano hilo ni mwendesha mashitaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai – ICC, ambayo imetoa hati za kukamatwa Rais wa Urusi Vladmir Putin na maafisa wa kijeshi wanaohuishwa na vita hivyo. Serikali ya Uholanzi imesema katika taarifa kuwa Uholanzi inaamini kuna umuhimu mkubwa kwamba ukweli na haki vipatikane kwa Ukraine na waathiriwa wote wa uchokozi wa Urusi.

Kwenye kongamano hilo, mfumo wa kulipa fidia kutokana uharibifu uliosababishwa na uvamizi wa Urusi umezinduliwa rasmi. Mchakato huo utawaruhusu watu kuwasilisha madai yao ya kulipwa fidia kwa uharibifu, vifo au mejeraha yaliyowakumba kutokana na uvamizi wa Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba
Ukraine inasema lazima mali zote za Urusi zikamatwe na kuwafaidi waathiriwa wa vita UkrainePicha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Baraza la Ulaya ambalo wanachama wake walianzisha Sajili hiyo mwezi Mei mwaka jana, ilisema katika taarifa kuwa uzinduzi huo wa leo unalenga madai ya uharibifu au uteketezaji wa mali. Limesema kati ya madai 300,000 na 600,000 yanatarajiwa kuwasilishwa.

Akizungumza pembezoni mwa kongamano hilo la mjini The Hague, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema hiyo ni hatua ya kwanza muhimu katika juhudi za kuiwajibisha Urusi. Waziri Kuleba ameongeza kuwa hii leo, maafisa wa Urusi na uongozi wa nchi hiyo huenda wanajihisi salama lakini kila siku kwenye uwanja wa mapambano, kwenye jukwaa la kimataifa, Ukraine inafanya juhudi za kuwapokonya hisia hiyo ya usalama.

Ujerumani kuipa Ukraine makombora

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

Wakati huo huo, Ujerumani kupitia wizara yake ya ulinzi imesema kuwa itaipa Ukraine makombora 180,000 kama mchango wake kwa mpango unaoongozwa na Czech wa kuinunulia Ukraine silaha, kwa kiasi cha euro milioni 576. Mwezi uliopita, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius alitangaza kifurushi cha msaada wa euro milioni 478 kwa Ukraine, bila kujumuisha msaada wa silaha unaoongozwa na Czech.

Kwenye uwanja wa mapambano, jeshi la Ukraine limesema droni za Urusi ziliilenga miundo mbinu ya nishati katika mashambulizi ya usiku kucha katika majimbo ya katikati mwa Ukraine ya Dnipropetrovsk na Kirovohrad. Gavana wa jimbo la Dnipropetrovsk amesema droni tisa zilidunguliwa ambako mabaki yalisababisha matukio mawili ya moto katika mji mkuu wa eneo hilo Dnipro. Lakini droni moja ilikipiga kituo kidogo cha umeme cha kampuni ya Ukrenergo katika jimbo la Kirovohrad, na kusababisha moto. Gavana wa eneo hilo amesema hakuna vifo wala majeruhi yaliyoripotiwa.

Shambulizi la droni la Ukraine
Shambulizi la droni ya Ukraine liliharibu bweni la wanafunzi katika eneo la Yelabuga, Tarkastan, UrusiPicha: Ostorozhno Novosti/Handout via REUTERS

Urusi imekuwa ikivipiga vituo vya nishati vya Ukraine katika wiki za karibuni, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa mfumo wa umeme wa Ukraine na hivyo kukatiza usambazaji umeme katika majimbo mengi.

Nao maafisa wa Urusi wamesema leo kuwa droni za Ukraine zilivishambulia viwanda katika mkoa wa Tatarstan, katika kile kinachoweza kuwa ni shambulizi la Ukraine lililoingia ndani zaidi ya mipaka ya Urusi tangu vita hivyo kuanza miaka miwili iliyopita. Watu saba walijeruhiwa katika shambulizi hilo karibu na miji ya Yelabuga na Nizhnekamsk karibu kilometa 1,200 mashariki ya Ukraine. Shambulizi hilo liliharibu bweni la wanafunzi na wafanyakazi katika eneo hilo la kiviwanda. Ukraine aghalabu huwa haikiri wala kukanusha kuhusika na mashambulizi kwenye ardhi ya Urusi.

reuters, ap, dpa