1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wa Msumbiji wana mawazo tofauti kutokana na malengo ya maendeleo ya milenia.

Sekione Kitojo1 Julai 2007

Kiasi cha watu asilimia 30 nchini Msumbiji wanafikiri kuwa hali zao za maisha zimekuwa bora tangu mwaka 2000 , mwaka ambao jumuiya ya kimataifa ilikubaliana juu ya malengo ya maendeleo ya milenia, MDGs, wakati kiasi cha watu asilimia 42 wanaamini kuwa hali haijabadilika.

https://p.dw.com/p/CHBp

Hii imejitokeza katika utafiti uliofanywa na shirika la utafiti ambalo ni asasi isiyo ya kiserikali, linalojumuisha asasi zisizo za kiserikali nchini Msumbiji ambazo zimeamua kuchunguza mtazamo wa umma kuhusu maendeleo kama yalivyoainishwa katika malengo hayo ya maendeleo ya milenia.

Mashirika hayo yasiyo ya kiserikali ni pamoja na kundi la madeni la Msumbiji na G20, muungano wa mashirika 20 yanayohusika katika mapambano dhidi ya umasikini. Yamesaidiwa na taasisi ya kaskazini na kusini, chombo cha utafiti chenye makao yake makuu nchini Canada kinachofanya utafiti kuhusu maendeleo.

Watafiti walifanya mahojiano na viongozi katika familia 6,750 katika maeneo ya vijijini na mijini katika nchi hiyo iliyoko katika eneo la kusini mwa Afrika mwezi wa Oktoba 2006, wakiwauliza vipi wao pamoja na familia zao wanavyoishi katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 na 2005.

Mahojiano hayo yalikuwa na lengo la kupata hali iwapo maendeleo yamepigwa kuelekea kufanikisha malengo hayo ya milenia.

Watu waliosema kuwa maisha yamekuwa bora wametoa sababu kuu kuwa ni mazingira mazuri ya kilimo. Wale waliosema kuwa maisha yako vile vile wametoa sababu ya kutokuwa na ajira. Kiasi cha watu asilimia 13 kati ya waliohojiwa wamesema kuwa serikali ya Msumbiji inapaswa kuchukua hatua zaidi ili kuboresha maisha ya raia zake.

Watu wanahisia kuwa serikali inaweza umuhimu zaidi katika biashara kuliko maisha ya watu. Serikali imefanya mengi katika uwanja wa biashara, amesema Fernando Menete, katibu wa kundi la madeni nchini Msumbiji , likiwa ni moja kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshirika katika zoezi hilo.

Wale waliohojiwa wanataka maendeleo zaidi katika usaidizi wa jamii, elimu na hospitali, miongoni mwa mengine.

Menete aliwasilisha utafiti huo katika mkutano wa taasisi za kijamii juu ya maendeleo , mkutano wa kimataifa wa siku tatu wa mashirika yasiyo ya kiserikali unaofanyika mjini Geneva, Uswisi, unaosimamiwa na mkutano wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika uhusiano wa mashauriano na umoja wa mataifa pamoja na kampeni ya milenia ya umoja wa mataifa.

Tatizo la ukosefu wa elimu ya msingi ni kubwa zaidi katika katika maeneo ya vijijini. Watu wa vijijini wana viwango vya chini vya elimu. Wanaacha shule kwasababu wanafikiri watapata kazi hata kama hawana elimu. Hawafahamu kuwa wanaweza kupata kazi nzuri zaidi iwapo watakwenda shule, ameeleza Menete.

Mtazamo wa watu unakwenda sambamba na takwimu za utafiti zinazoonyesha kuwa wanaume nchini Msumbiji bado wana nafasi zaidi kuliko wanawake. Wanawake wanajishughulisha zaidi na kilimo ama uzazi, amesema Menete. Tatizo kubwa kabisa ni lile la wasichana wadogo kupata uja uzito na mapema.

Hata hivyo nchi hiyo imefanya vizuri katika lengo la milenia la kupunguza vifo vya watoto kwasababu ya hatua zilizopigwa za kuimarisha huduma ya chanjo. Lakini pia hapa mwanya mkubwa ulionekana baina ya mijini na vijijini, ambako watu walikuwa bado wanahitaji kwenda mwendo mrefu kupata huduma za afya. Wengi wanaendelea kwenda kwa waganga wa kienyeji.