Washington. Hali ya hatari kitaifa yatangazwa.
23 Septemba 2005Kimbunga kinachojulikana kama Rita kimetangazwa kuwa ni hali ya hatari kwa taifa na utawala wa rais George Bush wa Marekani kabla ya kimbunga hicho kutua katika eneo la Texas mapema siku ya Jumamosi.
Kiasi cha watu milioni 1.8 wametakiwa kuondoka katika maeneo ya pwani ya Texas.
Gavana wa jimbo jirani la Louisiana , Kathleen Blanco pia amewataka wakaazi wa maeneo ya pwani kuondoka katika eneo hilo.
Kimbunga Rita ambacho kina upepo unaokwenda kwa kasi ya kilometa 240 kwa saa , ni kikubwa , kilichotanda katika nusu ya eneo la ghuba ya Mexico.
Katika njia itakayopitia kimbunga hicho kuna vinu vya kusafishia mafuta pamoja na kuhifadhia gesi vinavyotoa asilimia 23 ya mahitaji yote ya nishati nchini Marekani.
Vingi vimekwisha fungwa, na kusababisha upungufu mwingine kutoka ule uliosababishwa na kimbunga Katrina ambacho kilishambulia mji wa New Orleans wiki tatu zilizopita.
Bei ya mafuta mepesi ghafi duniani imepanda juu ya dola 65 kwa pipa.