Wanawake wa Afrika na olimpik | Michezo | DW | 30.07.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Wanawake wa Afrika na olimpik

Wasichana wa Ethiopia na Kenya watarajiwa kurudi na medali za dhahabu kutoka Beijing.

Michezo ya Olimpik ya Beijing,itafunguliwa rasmi wiki kutoka sasa.Miaka ya nyuma wanariadha wakike wa Afrika walikua hawafui dafu au walikuwa miongoni mwa wale wanaoitwa "also-runs"- miongoni mwa walioshiriki . Lakini, tangu mwanariadha wa kwanza wa kike wa Afrika kutawazwa bingwa wa Olimpik katika michezo ya Los Angeles, 1984-mmorocco Nawal el Moutawakel,wanawake wa Afrika wameanza kutia fora katika mashindano sio tu ya ubingwa wa riadha duniani kama yale ya mwaka jana huko Osaka,Japan, bali hata ya olimpik.

Hasa wasichana wa Kenya na Ethiopia wanatazamiwa kutamba katika michezo ya wiki ijayo Beijing-kuanzia mita 800 hadi 10.000 na marathon.

Miongoni mwa wasichana wa Afrika au wanaotarajiwa sana kurudi nyumbani na medali za dhahabu ni Mkenya Pamela Jelimo -mwenye umri wa miaka 18 na shoga yake bingwa wa dunia wa Osaka, Jeneth Jepkosgei katika mita 800.

Jelimo alianza kukimbia masafa ya mita 800 hapo April tu mwaka huu.Hapo kabla akifuata nyayo za mama yake ,Jelimo alikuwa akikimbia mbio za mita 400.Chipukizi huyu mpya kutoka Rift Valley,alitiwa shime si na mwengine bali mwenzake Janeth Jepkosgei na sasa amekua adui yake mkubwa lakini katika mashindano tu.Nje ya uwanja urafiki wao umebakia pale pale.

Jelimo amemshinda Jepkosgei mara zote 5 walizopambana katika medani ya riadha kuanzia Mei mwaka huu.

Sasa anatapia medali ya dhahabu katika michezo ya Beijing ili kuwa msichana wa kwanza wa Kenya kutawazwa bingwa wa olimpik.

Akishinda, atafuata nyayo za mwanamsumbiji Maria Mutola -bingwa wa olimpik wa Sydney, Australia, 2000 na sasa amestaafu.Jelimo anajivunia sana bingwa huyo wa Msumbiji alieshikilia rekodi ya Afrika ya mita 800 ambayo aliivunja Jelimo pale alipokua njiani kushinda mbio za masafa hayo za Golden League hapo Juni mosi, mjini Berlin,Ujerumani.

Mchuano kati ya shoga hawa wawili kutoka kenya: Pamela Jelimo na Janeth Jekosgei katika finali ya Olimpik huko Beijing, sio tu utaipatia Kenya medali ya dhahabu bali hata ile ya fedha.

Wasichana wa Ethiopia wamekuwa wakitoa changamoto kali kwa wakenya kama upande wa wanaume wafanyavyo akina Kenenisa Bekele na Gebreselassie:

Wasichana 2 wa Ethiopia wa masafa marefu ,bingwa wa rekodi za dunia mita 5000 na 10.000 Tirunesh Dibaba na shoga yake Meseret Defar,bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita 5000, ni hakikisho jengine la medali za dhahabu kwa wasichana wa Afrika mjini Beijing.

Dibaba, mwenye umri wa miaka 22- bingwa mara 2 wa dunia wa mita 10.000, huenda akakimbia masafa yote 2-mita 5000 na 10.000.La akiamua kukimbia mita 10.000 pekee, mwenzake Meseret Defar atatamba katika mita 5000.

Halafu kuna dada wa Tirunesh - Ejagayehu Dibabani bingwa wa medali ya fedha wa olimpik katika mita 10.000 wakati dada mwengine mchanga zaidi Genzebe akiwa na umri wa miaka 17 aliibuka bingwa wa mbio za nyika-cross-country-huko Edinburgh,Scotland mwaka huu.tirunesh Dibaba amesema baadhi ya wakati anafanya mazowezi pamoja na dada zake hao Genzebe na Ejegeyehu.

Amesema maandalio yao kwa olimpik yakienda uzuri.

Pale kikosi cha wanariadha wa Ethiopia kilipotangazwa mapema mwezi huu, Tirunesh Dibaba alitajwa atakimbia masafa yote 2-mita 500 na mita 10.000.

Wasichana wa Kenya na ethiopia wanatamba pia katika mbio za marathon na hata mita 3000 kuruka viunzi-mbio ambazo Kenya yadai ni mali yake.

Kwahivyo, iliosalia ni kungoja bunduki kulia kuona medali ngfapi za olimpik za dhahabu,fedha na shaba zitaletwa na wavulana na n gapi na wasichana wa Afrika kutoka michezo ya Beijing,2008.