1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

wanasiasia watoa miito ya kutatanisha nchini Irak

9 Julai 2007

Wanasiasa mashuhuri wa Kishia na wale wa Kisunni sasa wanawataka raia wa Irak wajihami kwa silaha kwa ajili ya kujilinda baada ya vurugu za mwishoni mwa wiki zilizo sababisha vifo vya zaidi ya watu 220.

https://p.dw.com/p/CB2y
Bendera ya irak
Bendera ya irak

Miito iliyotolewa na wanasiasa wa Irak inafuatia vurugu za siku za jumamosi na jumapili ambapo pia watu wengine 60 waliuwawa katika mfululizo wa mashambulio ya mabomu katika mji wa Baghdad.

Taarifa kutoka mjini Baghdad zinafahamisha juu ya ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu kutoka kwenye idara za ulinzi, usalama na wizara ya mamabo ya nje unaotarajiwa kuzuru Saudi Arabia hapo kesho kuwasilisha ombi la kuwepo ushirikiano katika juhudi za kupambana na ugaidi, hayo ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Irak Hoshyar Zebari.

Saudi Arabia ambayo ni nchi yenye nguvu miongoni mwa madola ya Kisunni katika mashariki ya kati imekuwa na wasiwasi na utawala wa Kishia nchini Irak kwa hofu kwamba huenda utawala huo ukawa una ushawishi mkubwa wa Iran.

Baadhi ya viongozi wa kidini wa Saudi Arabia wamekuwa wakiushutumu utawala wa Irak kwa madai kuwa utawala huo unawakandamiza Wasunni walio wachache huku kukiwa na tetesi kuwa fedha nyingi kutoka Saudia zinamiminika nchini Irak kuwaunga mkono wapiganaji wenye msimamo mkali.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Irak Hoshyar Zebari ameonya kuwa iwapo Marekani itazama katika shinikizo za kuyaondoa majeshi yake kwa haraka kutoka nchini Irak basi hatua hiyo huenda ikaitumbukiza nchi hiyo katika vurugu za wenyewe kwa wenyewe au hata ukazuka mzozo wa eneo zima la mashariki kati.

Zebari amesema kwamba anafahamu kwamba rais Bush anakabiliwa na miito ya kurejeshwa nyumbani askari wa Marekani kutoka nchini Irak lakini ametahadharisha kuwa askari wa Irak bado hawajawa na utayarifu wa kutekeleza majukumu ya kulinda usalama katika nchi hiyo inayokabiliwa na mzozo.

Rais Bush anaandamwa na pingamizi kali kutoka kwa chama cha upinzani cha Demokratik dhidi ya sera zake kuhusu Irak.

Wasaidizi wa Ikulu ya White House wanasema kuwa rais Bush anahitaji kubadili mfumo wake kwani baadhi ya wawakilishi wa baraza la Seneti wa chama chake cha Republikan hawaungi tena mkono sera za rais huyo.

Wakati huo huo kanda ya kaseti inayoaminika kuwa na sauti ya makamu wa kundi la aliyekuwa rais wa Irak Saddam Hussein imesema kuwa kundi lake litazidisha mapambano hadi pale wanajeshi wote wa kigeni watakapo ondoka kutoka nchini Irak na kuitaja Marekani kuwa imeshindwa katika vita hivyo vya Irak.

Sauti hiyo inayo aminiwa kuwa ni ya Izzat Ibrahim al Douri hata hivyo haijahakikishwa iwapo kweli ni yake, lakini Wairak wengi wamethibitisha kuwa wanaitambua sauti hiyo kuwa ni ya al Douri.

Al Douri alikuwa ni miongoni mwa maafisa wenye vyeo vya juu katika utawala wa Saddam Hussein ambae hajulikani aliko mpaka sasa, ametangaza masharti mengi hadi kufikia mwisho wa upinzani dhidi ya majeshi ya kigeni nchini Irak hii ikiwa ni pamoja na kuondoka kwa majeshi hayo, kukiri maovu yote yaliyofanyiwa raia wa Irak na kulipa fidia kwa hasara iliyotokea tangu Irak kuvamiwa.