1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ulaya kutua CAR mwezi Machi

14 Februari 2014

Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa kikosi chake kitakachopelekwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kitafanya hima kuunda ukanda salama katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, ambako raia wataweza kukimbilia na kujisikia salama.

https://p.dw.com/p/1B8NA
Kikosi kitakachopeleka kitaungana na wafaransa 1600 ambao tayari wako katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kikosi cha EU kitaungana na wafaransa 1600 ambao tayari wako katika Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: MIGUEL MEDINA/AFP/Getty Images

Maelezo hayo kuhusu majukumu kitakayokuwa nayo kikosi hicho cha Umoja wa Ulaya (EU) chenye wanajeshi 500, yametolewa na mtu aliyeteuliwa kuwa kamanda wa kikosi hicho, Meja Jenerali Philippe Ponties wa Ufaransa, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels.

Mbali na kuunda haraka eneo salama kuwapa hifadhi raia wanaokimbia ghasia, kikosi hicho cha Ulaya vile vile kitakuwa na jukumu la kuulinda uwanja wa ndege wa mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui. Watu takribani 100,000 wamekimbilia katika uwanja huo kuyanusuru maisha yao. Kamanda huyo amesema aliutembelea mji huo wiki iliyopita, na kutaja hali yake kuwa tulivu lakini yenye wasiwasi, na ambayo inaweza kubadilika haraka.

Uwezekano wa kuwasili mwezi ujao

Ingawa imeelezwa kuwa kikosi hicho kitapelekwa haraka iwezekanavyo, hakuna tarehe iliyotajwa ya kuwasili kwake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Baadhi ya maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema wana matumaini wanajeshi wao wataanza kutua mjini Bangui mwanzoni mwa mwezi ujao.

Rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-Panza
Rais mpya wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-PanzaPicha: Eric Feferberg/AFP/Getty Images

Bado haijulikani rasmi ni nchi gani zitachangia wanajeshi katika kikosi hicho, ingawa inafahamika kwamba nchi sita za Umoja wa Ulaya ziliahidi kuchangia wanajeshi na maafisa wa polisi. Ahadi hiyo ilitolewa jana katika mkutano uliofanyika mjini Brussels. Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamethibitisha kuwa Estonia, na nchi nyingine isiyo mwanachama wa Umoja huo, Georgea zimesema ziko tayari kutuma wanajeshi wao katika operesheni hiyo itakayogharimu euro milioni 26.

Ulaya ambayo kawaida husita kuwapeleka wanajeshi wake katika maeneo yaliyo na hatari ya dhahiri, iliitikia haraka wito wa Ufaransa kutaka msaada katika operesheni inayoendeshwa na wanajeshi wake 1600 ambao tayari wako Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Mataifa kuharakisha mambo

Sambamba na juhudi hizo za amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, rais wa Ufaransa Francois Hollande amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, akiutaka umoja huo kutafuta njia ya haraka kupeleka ujumbe wa amani kukomesha umwagaji damu wenye msingi wa kidini.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande akiwatembelea wanajeshi wa nchi yake mjini Bangui Desemba mwaka jana
Rais wa Ufaransa Francois Hollande akiwatembelea wanajeshi wa nchi yake mjini Bangui Desemba mwaka janaPicha: picture-alliance/AP

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia wakimbizi Antonio Guterres alionya kuwa hali ya kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikuwa ikidhoofika kwa kiwango kisichoelezeka. Kauli hiyo aliitoa baada ya kuuzulu mji mkuu wa nchi hiyo Jumatano wiki hii.

Wakati huo huo, mtu aliyejitangaza kiongozi wa wanamgambo wa kikristo wajulikanao kama anti-Balaka Richard Bejouane, alitupilia mbali onyo la rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bi Catherine Samba Panza, la kutangaza vita dhidi ya kundi hilo linalotuhumiwa kuwalenga waislamu.

Akizungumza na maelfu ya wanamgambo wa kundi lake mjini Bangui jana, Bejouane alisema kutangaza vita dhidi ya kundi lake ni sawa na kutangaza vita dhidi ya umma mzima wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Bejouane alidai kundi lao linao wanamgambo wapatao 52,000 ambao wako tayari kupokea amri, wakiwemo 12,000 katika mji mkuu peke yake.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo