1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAR yataka wanajeshi zaidi wa kulinda amani

Christina Ruta30 Januari 2014

Hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha wanajeshi wa Umoja wa Ulaya kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati imepokelwa vyema, lakini waangalizi wanasema idadi yao haitoshelezi kuhakikisha usalama unarejea.

https://p.dw.com/p/1AzLU
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Samba-Panza akiwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius.
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Samba-Panza akiwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius.Picha: Reuters

Uamuzi wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kutuma wanajeshi wa Umoja wa Ulaya kuingilia kati nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umepokelewa kwa kujizuwia. Kwa mujibu wa azimio la baraza hilo wanajeshi wapatao 600 wa Umoja wa Ulaya wamepewa mamlaka ya kurejesha usalama katika mji mkuu Bangui na kuhakikisha usalama wa raia, ikibidi hata kwa kutumia nguvu.

Ujumbe huo uliyopewa jina la EUFOR RCA - au Kikosi cha Umoja wa Ulaya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, kinapaswa kusaidiana na kikosi cha Ufaransa chenye wanajeshi 1,600 na kile cha Umoja wa Afrika MISCA, chenye jumla ya wanajeshi 4400 vilivyoko tayari nchini humo. Wanajeshi hao wa Umoja wa Ulaya wanaweza kukaa mjini Bangui kwa hadi miezi sita. Kisicho bayana hata hivyo ni lini wanajeshi hao wataanza kazi, na ni mataifa gani ya Umoja wa Ulaya yatachangia wanajeshi.

Wanajeshi wa Ufaransa walioko mjini Bangui.
Wanajeshi wa Ufaransa walioko mjini Bangui.Picha: Getty Images/AFP/Miguel Medina

Ujerumaji haiko tayari kutuma wanajeshi wake

Mbali na Mali, Somalia na eneo la pembe ya Afrika, kikosi hicho ndiyo ujumbe wa nne wa pamoja cha Umoja wa Ulaya barani Afrika. Ujerumani haiko tayari kutuma wanajeshi, lakini inaweza kuhakikisha usafiri wandege katika mataifa ya jirani. Wakati likiruhusu kuepelekwa kwa wanajeshi hao, baraza la usalama liliitaka serikali ya mpito mjini Bangui kuhakikisha kuwa inafanya uchaguzi haraka iwezekanavyo.

Waangalizi hata hivyo wana mashaka iwapo ujumbe huo utaweza kusitisha vurugu zilizolikumba taifa kwa miezi kadhaa sasa. Virginie Dero, mkurgenzi wa shirika la haki za binaadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, alisema katika mahojiano na DW kwamba wanahitaji wanajeshi zaidi.

"Kwa mgogoro tunaoushuhudia sasa, hata vikosi vya ufaransa na vile vya Misca haviwezi kuutuliza nchi. Tunahitaji wanajeshi zaidi. Kwa mfano ukiangalia mji wa Kabou, uko umbali wa kilomita 600 kutoka Bangui, na hakujaripotiwa uwepo wa wanajeshi hao katika eneo hilo. Na hadi hilo lifanyike, raia wanaendelea kushikiliwa mateka na makundi ya wanamgambo wa Seleka na anti-balaka," alisema.

Misca kuwa kikosi cha Umoja wa Mataifa?

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Panza-Samba, katika mahojiano na DW alikaribisha kutumwa kwa wanajeshi wa Umoja wa Ulaya, lakini aliomba msaada zaidi kutoka jumuiya ya kimataifa. "Hii huenda isitosheleze, lakini utakuwa mchango mzuri. Nimesema mara kwa mara kwamba vikosi vilivyopo havitoshi kurejesha utulivu Bangui na nchini kote. Tunahitaji wanajeshi zaidi na hivyo msaada wa Umoja wa Ulaya unakaribishwa sana," alisema rais huyo wa mpito.

Rais Panza alizungumzia hali ya kutisha ya usalama mjini Bangui, sambamba na maeneo ya ndani ya nchi, na kueleza matumaini yake kwa kikosi cha Misca kupanuliwa na kuwa kikosi cha Umoja wa Mataifa kwa kuongezewa maelfu ya wanajeshi. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa wanajeshi wasiopungua 10,000 wanahitajika ili kurejesha utulivu nchini humo.

Waziri mkuu wa mpito Andre Nzapayeke.
Waziri mkuu wa mpito Andre Nzapayeke.Picha: Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon bado hajawazia kupeleka ujumbe mkubwa kiasi hicho. Alitoa wito kwanza kwa mataifa ya Afrika kuimarisha ushiriki wake kijeshi na kifedha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jumamosi ya tarehe mosi Februari baada ya kukamilika kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, utafanyika mkutano wa kuchangia mataifa yenye migogoro kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Serikali mpya kutuliza uhasama?

Hata hivyo, rais hatoshiriki rasmi katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika, kwa sababu uanachama wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ulisimamishwa kufuatia mapinduzi ya waasi wa Seleka mwezi Machi mwaka jana. Rais wa Halmashauri ya Umoja huo Nkosazana Dlamini-Zuma, alisema siku ya Jumatano, kwamba rais Panza anaweza tu kushiriki tu kama mgeni wakati wa uwasilishaji wa ripoti kuhusu hali nchini mwake.

Habari njema ni kwamba hivi sasa, baada ya miezi kadhaa vurugu, kuna serikali mpya katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jumatatu ya tarehe 17. Januari, waziri mkuu wa muda Andre Nzapayeke alitangaza baraza lake la mawaziri 20, ambapo watatu yao ni Waislamu kutoka kutoka kundi la Seleka, na wengine ni Wakristu waliokaribu na wanamgambo wa anti-bakala.

Mwandishi: Matthaei Katrine
Tafsiri: Iddi Ismial Ssessanga
Mhariri: Saum Yusuf