1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wajazana kuvuka mpaka kati ya Uigiriki na Uturuki

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
2 Machi 2020

Polisi wa Ugiriki walitumia gesi ya kutoa machozi kuwakabili wakimbizi waliotaka kuingia nchini humo kutoka Uturuki. Kwingineko mtoto mmoja amekufa baada ya boti kuzama wakati boti ilipojaribu kuvuka mpaka wa baharini.

https://p.dw.com/p/3YlMF
Griechenland Grenzübergang bei Kastanies/Edirne
Picha: Reuters/A. Avramidis

Kifo cha mtoto huyo kilichoripotiwa na walinzi wa baharini ni cha kwanza baada ya wahamiaji wapatao 13,000, wakiwemo raia kutoka Syria, Afghanistan na Iraq kuanza kulundikana kwenye mpaka kati ya Uturuki na Ugiriki mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kutangaza hatua ya kulegeza vizuizi kwa wakimbizi waliokuwa wanataka kuvuka mpaka na kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Idara za Ugiriki zimesema, katika kipindi cha saa 24 zilizopita wakimbizi takriban alfu 10 walizuiwa kuvuka mpaka wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Watu 68 walikamatwa na kushtakiwa kwa kuingia nchini Ugiriki kinyume cha sheria.

Polisi wa Ugiriki walijaribu kuwazuia wakimbizi hao kwa kuwashambulia kwa gesi ya kutoa machozi wakati  baadhi wakiwa na mabango yaliyoandikwa maneno ya kusisitiza amani na kuomba kuruhusiwa kuingia nchini Ugiriki. Baadhi ya wakimbizi walijaribu kuingia kwenye visiwa vya Ugiriki kutoka kwenye pwani ya Uturuki.

Uamuzi wa rais Erdogan unamaanisha kuachana kabisa na sera ya hapo awali ya kuwadhibiti maalfu ya wakimbizi waliokuwamo nchini Uturuki. Hata hivyo Ugiriki imesema wazi kwamba mpaka wake utaendelea kufungwa.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der LeyenPicha: AFP/J. Thys

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanapanga kukutana wiki hii kwa ombi la Ugiriki ili kujadili hali hiyo, huku kukiwa na hofu ya kuongezeka msongamano wa wakimbizi hali ambayo ilisabaisha mikwaruzano ya kisiasa miongoni mwa nchi za Ulaya mnamo 2015.

Msemaji wa serikali ya Uigiriki, Stelios Petsas amesema nchi hiyo itaongeza doria katika mipaka ya ardhini na baharini upande wa kaskazini-mashariki na pia imesimamisha kushughulikia maombi ya wanaotaka hifadhi nchini humo kutoka kwa wakimbizi walioingia nchini humo kinyume cha sheria.

Maafisa watatu wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya watatembelea nchini Ugiriki katika eneo ambalo maelfu ya wakimbizi wanapitia kuja Ulaya ili kutathmini msaada unaoweza kutolewa. Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na Rais wa Bunge la Ulaya David Sassoli watakutana na Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Misotakis hapo kesho Jumanne kwenye mpaka kati ya Ugiriki na Uturuki. Tume hiyo pia itafanya mazungumzo na serikali ya Uturuki kuangalia mahala panapohitajika msaada kuhusu wakimbizi walio ndani ya Uturuki.

Vyanzo:/AP/RTRE/DPA