1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi mashariki mwa Congo wakabiliwa na uhaba wa chakula

John Juma
19 Februari 2024

Huku mzozo wa kiusalama ukizidi mashariki mwa Kongo, inaripotiwa kuwa maelfu ya wakaazi wa maeneo hayo wanang'ang'ania chakula.

https://p.dw.com/p/4cZgU
Maelfu ya watu wakimbia machafuko ya waasi wa M-23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Maelfu ya watu wakimbia machafuko ya waasi wa M-23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yametahadharisha kuwa mgogoro wa kibinadamu unatishia kuwa mbaya mashariki mwa Kongo ambako kuna zaidi ya watu milioni 5 waliokimbia vita kutoka mikoa minne ya eneo hilo. 

Mapigano yanayoendelea kuwa makali kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, yamevuruga usambazaji wa vyakula vya misaada katika mji wa Goma ulioko mashariki wa Kongo. Hali hiyo imewaathiri zaidi ya wakaazi milioni mbili pamoja na wakimbizi wa ndani.

Soma pia: Baraza la Usalama lahofia kuongezeka ghasia Mashariki ya Kongo

Tangu mwanzo wa mwaka huu, mapigano yamepamba moto katika miji na vijiji karibu na mji wa Goma ambao ndio mji mkuu wa mkoa huo, mnamo wakati waasi wakikamata baadhi ya viunga vya mji huo na hivyo kulazimisha maelfu ya raia kukimbilia mjini kwa usalama wao.

Matumizi ya zana nzito nzito za vita na mashambulizi yamewaua makumi ya raia. Aidha hospitali ndani ya mji wa Goma zinatatizika kuhudumia ongezeko kubwa la raia wanaojeruhiwa kwenye machafuko hayo.

Huku waasi wakiripotiwa kukaribia mji wa Sake, ulioko takriban kilomita 25 magharibi mwa Goma, wakaazi wa mji huo sasa wanategemea kiasi kidogo cha chakula kinacholetwa kutumia mitumbwi au boti ndogo kutoka vijiji vya Ziwa Kivu.

Sake, Mkoa wa Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Mkaazi wa Mashariki mwa Congo akikimbia machafuko pamoja na mifugo yake.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Machafuko yatatiza usafirishaji bidhaa za kilimo kufika Goma

Soko la Kituku lililoko kwenye kingo za ziwa hilo limekuwa chanzo muhimu cha chakula kwa mji wa Goma.

oma 

Esperance Nyota ambaye ni muuzaji wa ndizi katika soko hilo ametahadharisha  kuhusu njaa kubwa itakayojitokeza ikiwa machafuko hayo yataendelea na ikiwa njia za kusafirisha bidhaa za mashambani zitaendelee kufungwa.

Soma pia: UM wasema wafanyakazi wa MONUSCO wameshambuliwa Kinshasa

Hii itasababisha njaa kwa sababu watu wote wa Goma tunategemea barabara ya Minova kwa mazao ya kilimo. Lazima wafanye kila njia kuifungua barabara hii. Nina imani kuwa kufungua barabara hii kutatatua tatizo na kila kitu. Mamlaka za nchi lazima wafanye kila wawezalo kumaliza vita, amesema Nyota.

Serikali ya Kongo, maafisa wa Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zimeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, wanaodai kulinda masilahi ya jamii ya Watutsi dhidi ya wanamgambo wa Kihutu ambao viongozi wao walishiriki mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000.

Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo dhidi yake.

Wanawake waandamana kutaka vita kukomeshwa DRC

Rwanda yakataa wito wa Marekani kuitaka iondoe wanajeshi na mifumo yake ya makombora ndani ya DRC

Mnamo Jumamosi, Marekani iliihimiza Rwanda kuwaondoa mara moja wanajeshi wake walioko ndani ya Kongo na pia iondoe mifumo yake ya makombora ikisema, vinatishia maisha ya raia, ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine, vinatishia usalama wa maafisa wanaotoa misaada na usalama wa ndege za kibiashara zinazohudumu mashariki mwa Kongo.

Lakini mnamo Jumatatu, mamlaka nchini Rwanda ililikataa wito wa Marekani wa kuondolewa kwa wanajeshi na mifumo yake makombora.

Soma pia: Umoja wa Mataifa hatiani kuhusu unyanyasaji wa kingono DRC

Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilitaja vitisho kwa usalama wa raia wa Rwanda unaotokana na kuwepo kwa wanamgambo wenye silaha nchini Kongo.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wahamiaji, inakadiriwa kuwa takriban watu 135,000 wamekimbia Sake katika muda wa wiki moja iliyopita, na wanajiunga na mamia ya maelfu ya wahamiaji ambao wamekuwa Goma tangu mwaka 2022 kutokana na machafuko hayo.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba machafuko hayo ikiwemo mashambulizi ya kiholela ya mabomu yanatishia kuongeza shinikizo dhidi ya misaada haba iliyopo ya kuwashughulikia wahamiaji.

Chanzo: RTRE