Wajerumani hawaridhishwi na serikali ya Kansela Merz
24 Novemba 2025
Asilimia 22 pekee ya waliohojiwa ndio wanaoridhishwa na serikali ya muungano inayoongozwa na kansela Friedrich Merz, ikiwa chini kwa nukta mbili ikilinganishwa na utafiti uliofanyika Novemba 7.
Asilimia 67 bado hawajaridhishwa na serikali ya Merz huku asilimia 11 ikikataa kutoa maoni.
Taasisi hiyo iliwahoji watu 1,004 kati ya Novemba 20 na 21 na iliwauliza iwapo wanaridhia kazi ya Merz kama Kansela na iwapo pia wanaridhishwa au kutoridhishwa na serikali yake.Asilimia 25 ilipitisha na kuipenda kazi ya Merz, asilimia 64 haijaridhika nayo huku asilimia 11 ikikataa kutoa maoni.
Haya yanajiri wakati Merz mwezi uliopita alikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wabunge wa upinzani, juu ya kauli yake ya kufukuzwa kwa wahamiaji yaliyotafsiriwa kuwa ya kibaguzi. Merz alitoa kauli hiyo wakati akijibu suali kuhusu ushawishi wa chama cha siasa kali AfD na juhudi za serikali yake kurekebisha sera ya uhamiaji.
Steinmeier: Itikadi kali za mrengo wa kulia ni kitisho kwa demokrasia
Ripoti ya INSA imetolewa wakati hivi karibuni rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alionya kuwa ongezeko la itikadi kali za mrengo wa kulia na ubaguzi dhidi ya wayahudi vinazidi kutishia demokrasia nchini humo.
Steinmeier alizungumzia kuhusu ongezeko la siasa kali za mrengo wa kulia katika mfumo wa chama kinachopinga wahamiaji cha Alternative for Germany (AfD), ambacho kilipata asilimia 20.5 ya kura katika uchaguzi mkuu wa Februari na kushika nafasi ya pili.