1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri juu ya Iran, Thailand na muungano mkuu

Admin.WagnerD14 Januari 2014

Makubaliano ya muda kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, maandamano nchini Thailand na malumbano ndani ya serikali ya muungano mkuu ni miongoni mwa mada walizozungumzia wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1AqAS
Bangkok Proteste 29.11.2013
Maandamano ThailandPicha: Reuters

Mhariri wa gazeti la Handelsblatt anazungumzia juu ya makubaliano ya mataifa makubwa sita na Iran kuhusu mpango wa nyuklia wa taifa hilo la Kiislamu kwa kusema:

Hakuna mbadala kwa makubaliano ya sasa yaliyofikiwa na utawala mjini Tehran. Makubaliano hayo yana maana kubwa sana kwa utulivu wa mataifa ya kanda ya Ghuba na ulimwengu wa Kiislamu.

Ujerumani inapaswa kujihisi kuwa na jukumu kubwa la kisiasa na kiuchumi katika kufanikisha hilo, kwa sababu hakuna anayenufaika zaidi katika kanda hiyo kama makampuni ya Kijerumani, lakini pia Ujerumani inatizamwa kama mpatanishi anaetoa haki.

Ujerumani inapaswa yenyewe kujipa jukumu muhimu katika mchakato huo, kwa sababu washirika wake wamekuwa wakiiomba hilo muda mrefu.

Mhariri wa gazeti la Frankurter Rundschau naye anazungumzia makubaliano hayo ya Iran na mataifa makubwa na anasema huu ndiyo mwanzo wa kukaribiana na sasa makubaliano ya kudumu yanapaswa kuanza kujadiliwa mara moja.

Mhariri wa gazeti la gazeti la Straubinger Tagblatt anazungumzia maandamano yanayoendelea nchini Thailanda kwa kusema:

Nchi hiyo inakosa desturi ya demokrasia, hasa mahakama huru ambayo inaweza kuwaweka watala katika nafasi zao. Tabaka la watu wachache wa daraja la juu hawataki kuheshimu utawala wa walio wengi.

Wasomi wa mijini, tangu mamilionea, maafisa wa serikali na watu wa daraja la kati wanaridhika na serikali yao pale tu wanapokuwa wao ndiyo wenye sauti.Kuna pengo kubwa kati ya wakaazi wa mijini na vijijini, ambao ni maskini wa kutupa, huku wakaazi wa mji mkuu wakishikilia misaada kwa anasa.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe pia viko karibu kwa sababu pande zote haziko tayari kukaribiana. Hoja ya kuondoa rushwa ni kichekesho kwa sababu hata wapinzani wenyewe mifuko yao imekaa kiuchumi pale fursa itakapojitokeza.

Wahariri wa magazeti ya Berliner na Stuttgarter wametoa maoni yao juu ya malumbano ndani ya serikali changa ya muungano mkuu.

Mhariri wa Berliner Zeitung anasema serikali hiyo inapaswa kupimwa kutokana na kile walichokifanya au ambacho hawajakifanya. Anasema ni muhimu wapewe muda wafanye jambo kwanza.

Naye mhariri wa Stuttgarter Zeitung juu ya mada hiyo anasema:

Wale ambao wanachanganya muungano mkuu wa utawala na muungano wa kisiasa bila shaka watakataa tamaa. Hatua ya vyama vya muungano wa CDU/CSU kuunda serikali serikali na chama cha SPD ilitokana na kubadilika kwa urari wa madaraka ndani ya bunge kama walivyoamua wapiga kura na si kutambua ghafla kwa vyama hivyo vilivyokuwa na ilani zinazokinzana kwamba wanaweza kufanya kazi kwa maelewano. Chama Cha SPD si cha kulaumiwa sana kutokana na uzoefu wake mbaya na muungano mkuu uliopita. Lakini hatimaye kitakachokuwa muhimu ni kile ambacho wamefanikisha pamoja kama serikali na si kile walichotofautiana.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/Straubinger Tagblatt, Frankurter Rundschau, Handelsblatt, Berliner, Stuttgarter zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef