1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ipi athari ya vita vya Ukraine kwenye uchaguzi wa Ufaransa?

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
14 Aprili 2022

Athari ya vita vya Ukraine inaweza kuonekana katika uchaguzi wa rais nchini Ufaransa. Rais Emmanuel Macron na mpinzani wake Marine Le Pen wanatoa hoja tofauti katika kampeni zao.

https://p.dw.com/p/49x6d
Frankreich | Erste Runde der Präsidentschaftswahlen 2022 | Marine Le Pen und Emmanuel Macron
Picha: Paulo Amorim/IMAGO

Mgombea urais wa mrengo mkali wa kulia, Marine Le Pen, ana uhusiano wa karibu na Urusi na analemea upande ambao unalenga kuudhoofisha Umoja wa Ulaya na Jumuya ya NATO, hali ambayo inaweza kupunguza jitihada za nchi za Magharibi katika kuvikomesha vita vya nchini Ukraine. Le Pen anachuana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayeelemea mrengo wa siasa za kati ambaye mpaka sasa anaongoza kwa asilimia ndogo dhidi ya Le Pen kulingana na kura za maoni kabla ya uchaguzi wa marudio utakaofanyika mnamo April 24 nchini Ufaransa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AFP

Kuihami Ukraine

Serikali ya Macron imepeleka silaha nchini Ukraine za thamani ya euro milioni 100 katika wiki za hivi karibuni na imesema itapeleka silaha zaidi kama sehemu ya juhudi za kijeshi za nchi za Magharibi. Ufaransa imekuwa chanzo kikuu katika kupelekwa msaada wa kijeshi nchini Ukraine tangu mwaka 2014, baada ya Urusi kulitwaa eneo la Crimea mnamo mwaka 2014 na pia hatua yake ya kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga huko mashariki mwa Ukraine.

Le Pen ameelezea kutoridhishwa kwake kuhusu kupelekwa silaha zaidi nchini Ukraine. Amesema akichaguliwa, kama rais, ataendeleza msaada wa ulinzi na kijasusi lakini atakuwa na busara zaidi kuhusu kupeleka silaha nchini Ukraine kwa sababu anafikiri shehena hizo zinazopelekwa Ukraine zinaweza kuzitumbukiza nchi nyingine kwenye mzozo na Urusi.

Le Pen amesema vita vya Ukraine kwa kiasi vimebadilisha mawazo yake juu yar ais wa Urusi Vladmir Putin, lakini amesema anaamini kwamba nchi za Magharibi zinapaswa kujaribu kurejesha uhusiano na Urusi mara baada ya mzozo kumalizika. Amependekeza juu ya kuanzishwa anachokiita ``maelewano ya kimkakati'' kati ya NATO na Urusi ili kupunguza ushirikiano wa karibu kati ya nchi hiyo na China.

Marine Le Pen mgombea katika uchaguzi wa rais nchini Ufaransa
Marine Le Pen mgombea katika uchaguzi wa rais nchini UfaransaPicha: Michel Spingler/AP Photo/picture alliance

Kudhoofishwa Jumuiya ya NATO na Umoja wa Ulaya

Wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ni mlinzi shupavu wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na hivi karibuni aliimarisha ushiriki wa Ufaransa katika operesheni za NATO katika nchi za Ulaya Mashariki, Le Pen anasema Ufaransa inapaswa kujiweka mbali na miungano ya kimataifa na badala yake ipange na kufuata njia zake yenyewe. Anapendekeza kuiondoa Ufaransa kutoka kwenye Jumuiya ya kijeshi ya NATO, ambayo anafikiri inawatumia wanajeshi wa Ufaransa nje ya eneo ambalo wanastahili kuwemo hali ambayo itaifanya nchi hiyo kupoteza mvuto wake ndani ya muungano wa Magharibi.

Chanzo: AP