1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yafukuza wakimbizi

Abdu Mtullya2 Aprili 2016

Shirika la kutetea haki za binadamu duniani, Amnesty International linadai kuwa na ushahidi unaoonyesha kwamba Uturuki imewarudisha nyumbani wakimbizi wa Syria kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/1IOLF
Symbolbild Deutschland Flüchtlinge werden in Friedland erwartet
Picha: picture-alliance/dpa/S. Rampfel

Shirika hilo limesema maafisa wa Uturuki wamekuwa wanawakamata na kuwarudisha wakimbizi wa Syria katika makundi ya watu mia mia, wanaume, wanawake na watoto kila siku, tangu katikati ya mwezi wa Januari.

Wengi miongoni mwa wakimbizi hao walikuwa wale ambao hawakusajiliwa rasmi. Hata hivyo asasi ya Amnesty International imedai kuorodhesha mikasa ya wakimbizi waliofukuzwa ambao walikuwa wamesajiliwa.

Watu hao walirudishwa nchini Syria kwa sababu hawakuwa na hati zao za usajili wakati walipokamatwa.

Wakimbizi wauliwa kwa kupigwa risasi

Wakati huo huo shirika la Syria la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London limesema limepata ushahidi unaonyesha jinsi wakimbizi 16 walivyopigwa risasi na kufa ,wakati walipokuwa wanajaribu kuuvuka mpaka wa Syria ili kuingia Uturuki.Lakini shirika hilo linaamini idadi ya waliouawa inaweza kuwa kubwa zaidi.

Hatua iliyochukuliwa na Uturuki inadhihirisha hatari kubwa inayowakabili wakimbizi wanaorudishwa kutoka Ulaya, kutokana na mkataba uliofikiwa baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kuanza kutekelezwa wiki ijao.

Uturuki ilikubaliana na Umoja wa Ulaya juu ya kuwarudisha wakimbizi wanaoingia Ugiriki, kinyume cha sheria kuanzia mwezi huu. Na kwa kuyatekeleza makubaliano hayo Uturuki itapatiwa msaada wa fedha . Pia mchakato wa kuwaruhusu raia wa Uturuki kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya bila ya visa utaharakishwa.

Amnesty International Symbolbild
Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Aidha mazungumzo juu ya Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya yataharakishwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa.

Hata hivyo uhalali wa mkataba huo unategemea, iwapo Uturuki ni nchi salama kwa watu wanaoomba hifadhi ya ukimbizi, lakini katika ripoti yake shirika la kutetea haki za binadamu,Amnesty International limesema ni wazi kwamba nchi hiyo si salama kwa wanaoomba hifadhi ya ukimbizi.

Shirika la Amnesty International limesema kurudishwa kwa nguvu nchini Syria kwa watoto watatu bila ya wazazi wao pamoja na mwanamke mjamzito ni miongoni mwa mikasa lililoorodhesha.

Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imekanusha madai kwamba imewarudisha kwao wakimbizi wa Syria bila ya hiyari zao.

Wizara hiyo imesema Uturuki imekuwa inaitekeleza sera ya milango wazi kwa wakimbizi wa Syria kwa muda wa miaka mitano iliyopita na pia imeizingatia kanuni ya kutowarudisha wakimbizi katika nchi ambako wanaweza kuwamo katika hatari ya kuandamwa.

Ujerumani kuchukua wakimbizi

Wakati huo huo Ujerumani imesema itawachukua wakimbizi wa kwanza wa Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani amearifu kuwa idadi kubwa ya wakimbizi hao wanaotarajiwa kuanza kuwasili Jumatatu ijayo ni familia zenye watoto.

Kwa mujibu wa utaratibu uliokubaliwa pamoja na Umoja wa Ulaya kwa kila mkimbizi wa Syria ataekepewa hifadhi kihalali barani Ulaya,mwengine atachukuliwa na Uturuki kutoka Ugiriki.

Lakini shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema kurudishwa kwa nguvu kwa wakimbizi wa Syria kunaonyesha kasoro zilizomo katika makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afpe,dpa,

Mhariri: Yusra Buwayhid