Upinzani nchini Kyrgystan waunda serikali ya mpito | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Upinzani nchini Kyrgystan waunda serikali ya mpito

Umoja wa Ulaya umejitolea kuipa msaada wa dharura nchi ya Kyrgyzstan kurudisha hali ya amani nchini humo baada ya mapinduzi ya serikali.

Kiongozi wa upinzani nchini Kyrgystan Roza Otunbayeva

Kiongozi wa upinzani nchini Kyrgystan Roza Otunbayeva

Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo, Catherine Ashton, amesema kwamba umoja huo upo tayari kutoa msaada wa kibinadamu iwapo utahitajika, na kwamba umoja huo unafanya mazungumzo na washirika wake wengine kutafuta hatua za kuchukua dhidi ya hali ilivyo hivi sasa nchini Kyrgyzstan.

Catherine Ashton ameongeza kwamba kuna haja ya pande mbili husika kuwa tayari kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu ya migogoro iliopo na kusaidia kuleta umoja na ustawi wa nchi ya hiyo.

Bibi Ashton ameeleza kwamba ni muhimu kuweza kujua ni kwa jinsi gani nchi hiyo itaweza kurejesha amani na uongozi wake wa kidemokrasia na kikatiba.

Afisa mmoja wa wizara ya afya nchini humo ameripoti kufariki kwa watu takriban 75, huku wengine zaidi ya 1000 wakijeruhiwa kufikia sasa, kufuatia vurugu hizo zilionza tangu jana nchini humo.

Vurugu hizo zinasemekana zimesababishwa na wananchi kutoridhishwa na ongezeko la viwango vya ufisadi nchini humo na kupanda bei za bidhaa mara kwa mara jambo ambalo linatokea kwa nchi inayosemekana kuwa thuluthi ya wakaazi wake milioni 5.3 ni maskini.

Kufuatia hayo, na pia baada ya upinzani nchini Kyrgyzstan kutangaza hii leo kwamba umechukua uongozi wa serikali ya nchi hiyo, rais Kurmanbek Bakiyev amelazimika kuukimbia mji mkuu wa nchi hiyo alimokuwa.

Upinzani nchini humo umetangaza pia kuvunjwa bunge na baraza la mawaziri, huku wakiitisha waungwe mkono kidiplomasia kufuatia kuzuka kwa machafuko hayo.

Waziri wa zamani wa nchi za nje nchini humo, Roza Otunbayeva, ambae kwa sasa ametangazwa kuwa kiongozi wa muda, ameeleza kwamba rais wa nchi hiyo amekimbilia maeneo ya kusini mwa nchi hiyo kujaribu kutafutwa aungwe mkono.

"Kama ilivyo wizara ya usalama wa taifa na ile ya ndani sasa pia iko mikononi mwa uongozi wa maafisa wapya. Lazima tudhibiti uongozi na usalama, ndio kipa umbele."

Huku hayo yakijiri, shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch nchini Marekani, limetoa wito kwa serikali ya mpito ya nchi hiyo kuheshimu haki za binaadamu wakati huu.

Andrea Berg ambaye ni mtaalam wa shirika hilo, anasema kwamba hata nyakati za vurugu katika maeneo mbalimbali, viongozi walio mamlakani kwa wakati huo hawana budi kuhakikisha kwamba haki hizo zinadumishwa.

Andrea Berg anasema kwamba ni lazima kwa serikali ya mpito nchini humo kuhakikisha haki ya kuishi, kupiga marufuku mateso, haki za uhuru na usalama wa binaadamu na kushtakiwa watu, kihaki, yote haya yanadumishwa kwa wakati huu.

Kyrgyzstan imekuwa ikikumbwa na visa vya ufisadi na mtikisiko wa ustawi, na machafuko haya yametokana na hasira za upinzani kutokana na udanganyifu na makosa yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa urais nchini humo mwaka jana.

Mwandishi :Maryam Abdalla/AFPE/DPAE/RTRE.

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 08.04.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Mqbh
 • Tarehe 08.04.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Mqbh
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com