UNESCO yaamua Februari 13 iwe siku ya ″Redio Duniani.″ | Masuala ya Jamii | DW | 11.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

UNESCO yaamua Februari 13 iwe siku ya "Redio Duniani."

default

Kupotea kwa umuhimu wa Redio ni jambo lililokuwa likitabiriwa kwa miaka mingi, lakini ukweli ni kwamba kuachana na matumizi ya Redio litakuwa jambo la gharama kubwa kwa maendeleo.

Mirta Louren mkuu wa kitengo cha maendeleo ya vyombo vya habari katika shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa mataifa, UNESCO, anasema Redio ni rahisi, haina shida kuibeba na ina manufaa makubwa katika ukuaji kieneo na kitaifa.

Shirika hilo la Umoja wa mataifa lenye makao yake makuu mjini Paris, liliidhinisha wiki hii lile pendekezo la Uhispania kuitangaza siku ya Redio Duniani kila mwaka na ambayo imepangwa kuwa Februari 13 na ambayo itaadhimishwa kwa namna mbali mbali na wanachama 195 wa shirika la elimu,sayansi na utamaduni la umoja wa mataifa.

Lengo la Unesco ni kukuza na kuimarisha radio za kijamii na kusherehekea huduma inayotokana na Redio, katika wakati ambapo hadi sasa mchango na huduma ya Redio kwa binaadamu hadi sasa halikuwa jambo lililothaminiwa.

Wakati wa mkutano wa wiki mbili wa Unesco uliomalizika Alhamisi iliopita, nchi wanachama zilikubaliana juu ya malengo ambayo ni pamoja na kuleta mwamko kuhusu umuhimu wa Redio na hasa kwa jamii na vikundi vilivyotengwa .

Shirika la Unesco linasema kwamba kiasi ya watu bilioni moja au mtu mmoja katika kila saba duniani bado hawana uwezo wakuwa na Redio. Bibi Louren anasema kuna haja ya kuutanua uwezeakano wa mtu kuweza kumiliki Redio, kwa sababu kwa njia moja au nyengine hakuna chombo kinachoweza kuchukua nafasi ya Redio.

Akaongeza kuwa siku ya Redio duniani, itatumiwa kusisitiza juu ya haja ya kuzipa sauti jumuiya za kiraia na kutoa mwamko juu ya haki ya kuwasiliana kuimarisha mawasiliano miongoni mwa watangazaji na pia kukuza haki za binaadamu na za kiraia.

Kwa upande mwengine Redio imekuwa ikitumiwa vibaya kwa malengo ya propaganda wakati wa vita vya dunia na pia kuchochea machafuko kama ilivyotokea wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994.

Shirika la UNESCO limeandaa mpango kabambe, ukiungwa mkono na Sweden, ili kuimarisha Redio maeneo ya vijijini barani Afrika ili watangazaji waweze kuandaa vipindi vya manufaa kuhusu masuala yanayowagusa wakaazi wa vijijini, ikiwa ni pamoja na Kilimo na huduma ya afya.

Stesheni za Redio zitakazoendeshwa na akina mama wa vijijini zitakuwa sehemu ya mradi huo, na pia elimu jinsi ya kutumia teknolojia ya mawasiliano kama ujumbe wa maandishi utakaowafikia wasikilizaji ili waweze kutoa maoni au kuuliza maswali.

Mwandishi mmoja wa habari na mtangazaji Redio wa zamani, Jamion Knight, mkaazi wa Paris, aliyefanya kazi huko Caribbean, anasema Kutokana na kile alichokiona katika nchi nyingi zinazoendelea, Redio kwa jumla ndiyo aina rahisi kabisa ya kupata habari kwa watu ambao hawana uwezo wa kununua gazeti kila siku au uwezo wa kumiliki televisheni.

Redio pia inaweza kutumiwa kuwarekebisha wafungwa na kuwasaidia kurudi kuwa raia wema. Mfano mmoja wapo ni kuanzishwa kwa " Redio ya magereza," katika eneo la Caribbean ya kwanza ya aina yake. Wote-wafungwa na askari magereza walipewa mafunzo ya kuendesha vipindi, katika mradi uliogharimiwa na shirika la maendeleo ya kimataifa la Canada.

Hata hivyo haijafahamika wazi ikiwa mpango huo na mengineyo itaweza kutekelezwa, kutokana na matatizo ya fedha yanaiyolikabili Shirika la elimu,sayansi na utamaduni la Umoja wa mataifa-UNESCO kwa wakati huu.

Kutokana na Marekani kutangaza inapunguza mno mchango wake baada ya Palestina kukubaliwa uwanachama katika Unesco, Gabon imetoa mchango wa dola milioni mbili na UNESCO imeanzisha mtandao rasmi ambapo kwa jumla utaweza kutoa michango yao.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/IPS

Mhariri: Miraji Othman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com