Umwagikaji mafuta katika Ghuba ya Mexico. | Masuala ya Jamii | DW | 16.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Umwagikaji mafuta katika Ghuba ya Mexico.

BP yafanikiwa katika majaribio ya kwanza ya kusitisha kabisa umwagikaji wa mafuta.

Picha ya video inayoonyesha kusita umwagikaji mafuta katika Ghuba ya Mexico.

Picha ya video inayoonyesha kusita umwagikaji mafuta katika Ghuba ya Mexico.

Kampuni ya mafuta nchini Uingereza - BP imesema imefanikiwa kwa mara ya kwanza kusitisha kwa muda, umwagikaji mafuta uliokuwa ukiendelea kwa miezi mitatu sasa katika ghuba ya Mexico, kwenye majaribio ya kwanza ya kusitisha kabisa umwagikaji wa mafuta hayo.

Makamu mkuu wa rais wa kampuni hiyo ya mafuta ya BP,Kent Wells, alitangaza hapo jana muda mchache baada ya ma injinia kufanikiwa kuzifunga paipu tatu za mwisho za mfuniko mpya uliotumika kufunika kisima cha mafuta hayo, mwendo wa saa 20.25 usiku kwa saa za Afrika mashariki,kuwa mafuta hayo yamesita kumwagika katika bahari.

Wells, aliwaambia waandishi wa habari kuwa alifurahishwa na kusita umwagikaji huo, lakini alitoa tahadhari kuwa ndio mwanzo tu wa majaribio ya siku mbili, kukagua hali ya kisima hicho cha mafuta.

Huku naye Afisa mkuu wa shughuli za uendeshaji kampuni hiyo Doug Suttles anasema ni matumaini mazuri lakini alitahadharashisha kuwa huenda umwagikaji huo ukaanza tena.

Tangazo hilo ni ishara ya matarajio kwa wakaazi wa eneo hilo la pwani waliokimbia makaazi yao yalioharibiwa na uchafuzi huo wa mkubwa wa mazingira uliowahi kutokea katika historia ya Marekani.

Golf von Mexiko

Wafanyikazi wa BP wakisafisha fuo za bahari,Alabama.

Maeneo ya uvuvi yamefungwa huku watalii wametishiwa na kulazimika kuondoka,ikiwa hivi ndio vitega uchumi vikuu vya eneo hilo la kusini linalojaribu kuimarika baada ya mkasa wa kimbunga Katrina kilichotokea mnamo mwaka 2005.

Viumbe vya baharini vilivyo katika hatari ya kupotea pia vimetishiwa na mafuta mengi yanayomiminika katika fuo za bahari za majimbo matano,Texas,Louisiana,Mississipi,Alabama na Florida, huku shughuli za usafishaji wa fuo hizo zikisemekana kusalia kwa miaka kadhaa ijayo.

Serikali ya Marekani,kupitia rais Barack Obama ,ambayo imekuwa ikiishinikiza BP kusitisha umwagikaji mafuta hayo, imepokea vyema tangazo hilo la kufanikiwa kufunikwa kwa kisima hicho cha mafuta,lakini rais Obama pia alitahadharisha kuwa bado ni majaribio tu. Kiongozi huyo anatarajiwa kuzungumzia tena suala hilo hii leo.

Majaribio hayo yananuiwa kubaini iwapo kisima hicho cha mafuta kilicho na upana wa kilomita 4, kiliharibika wakati wa mripuko katika jukwaa la uchimbaji mafuta lililokodishwa na kampuni hiyo ya BP kutoka kampuni ya DeepWater Horizon,uliotokea tarehe 20 mwezi Aprili mwaka huu.

BP inatarajia kutoa mafuta katika kisima hicho yanayokisiwa kuwa mitungi kati ya 35,000 na 60,000 kwa siku. Lakini kufanya hivyo kutoka juu, kutalazimisha mafuta kumwagika upya iwapo kutakuwa na tundu nyingine zitakazokuwepo iwapo kisima hicho kiliharibika wakati wa mripuko huo.

Mkasa huo umeigharimu BP dola bilioni 3 unusu mpaka sasa, na malalamiko ya wakaazi wa maeneo athirika kutaka kulipwa fidia huenda yakazidisha viwango hivi mara 10 zaidi.

Kwengineko gazeti la Financial Times limeripoti kuwa BP inaharakisha uuzaji wa rasilmali zake zenye thamani ya hadi kufikia dola bilioni 20, ili kujiongezea fedha baada ya mkasa huo,na kuunda hazina ya thamani ya dola bilioni 20 hizo, kugharamia usafishaji wa maeneo athirika na umwagikaji mafuta hayo.

Mwandish:Maryam Abdalla

Mhariri:Josephat Charo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com