Umoja wa Mataifa wawekea wafadhili wa ugaidi vikwazo | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa wawekea wafadhili wa ugaidi vikwazo

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limewawekea vikwazo watu kadhaa wanaohusishwa na itikadi kali, wakiwemo wapiganaji wa kigeni, wafadhili na wanaowasajili wapiganaji hao kujiunga na makundi ya wanamgambo wa kijihadi

Watu binafsi kutoka Ufaransa, Saudi Arabia, Norway,Senegal na Kuwait ni miongoni mwa waliolengwa na kamati ya baraza la usalama la umoja wa Mataifa ya kupambana na Al Qaeda ambayo imetangaza vikwazo vya marufuku ya kuuziwa silaha, kutosafiri na kuzuiwa kwa mali zao.

Ufaransa iliwasilisha majina ya watu watatu kwenye kamati hiyo huku Marekani ikiwasilisha majina ya watu kumi na mmoja na makundi ya Ansar al Sharia na kikosi cha Abdaallah Azzam yaliyoko Tunisia yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ambayo yanawasajili vijana wa Tunisia kwenda kupigana Syria.

Marekani inafanya kampeini ya kijeshi dhidi ya IS

Hatua hiyo iliyochukuliwa na kamati hiyo ya baraza la usalama la umoja wa Mataifa inasadifiana na kutarajiwa kupitishwa kwa azimio hii leo katika mkutano wa baraza hilo utakaoongozwa na Rais wa Marekani Barrack Obama linalokusudia kuwabana wapiganaji wa kigeni wenye itikadi kali.

Rais wa Marekani Barrack Obama

Rais wa Marekani Barrack Obama

Hayo yanakuja wakati Rais Obama akiwa ameanzisha kampeni ya kuiunganisha Marekani na nchi washirika kukabiliana na wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita dola la kiislamu ambao wanayadhibiti maeneo mengi nchini Iraq na Syria na kuwahimiza wafuasi wao kuwashambulia raia wa nchi kadhaa duniani.

Miongoni mwa waliowekewa vikwazo na kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa ni Abd al-Rahman Muhammad al Qaduli raia wa Iraq ambaye ni afisa wa ngazi ya juu wa dola la kiislamu nchini Syria na ambaye awali alihudumu kama naibu wa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda nchini Iraq Abu Musab al Zarqawi.

Mwingine aliyewekewa vikwazo ni raia wa Norway Anders Cameroon Ostensvig Dale. Dale anatajwa kuwa mwanachama wa Al Qaeda katika rasi ya arabuni ambaye alifanya ziara kadhaa nchini Yemen alipopewa mafunzo ya kutengeza mikanda ya mabomu,viripuzi na mabomu ya kutegwa garini.

Azimio kupitishwa kuwabinya magaidi

Kulingana na Umoja wa Mataifa,uwezo wa Dale kusafiri nchi nyingi bila ya vikwazo vya kuhitajika hati za usafiri kunatoa fursa kwa tawi la Al Qaeda la rasi ya arabuni kumtumia kufanya mashambulizi katika nchi hizo.

US Angriffe auf IS Stellungen 23.09.2014

Moja ya ndege za kijeshi ilizozishambulia ngome za wanamgambo Syria

Shafi Sultan Mohammed al Ajmi raia wa Kuwait pia yumo katika orodha hiyo. Anaaminika huchangisha fedha kulifadhili kundi la wapiganaji la Al Nusra na hufanya kampeni katika mitandao ya kijamii kutafuta ufadhili wa wapiganaji wa Syria.

Wanadiplomasia wamesema baraza la usalama limekubali mswada wa azimio kutoka Marekani ambalo linatakupitishwa hii leo likidhamiria kuzuia usajili wa wapiganaji,kusafirisha au kuwapa silaha watu wanaopanga au wako tayari kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Kiasi ya wapiganaji 12,000 wamesafiri kutoka takribani nchi 74 kuelekea Syria na Iraq kujiunga na makundi yenye itikadi kali.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com