Ulinzi zaidi kwa watoto katika maeneo ya mizozo | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ulinzi zaidi kwa watoto katika maeneo ya mizozo

Karibu tangu miaka 20 sasa, watoto wako katika hifadhi maalum ya jamii ya kimataifa pale ulipoanza kufanya kazi mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kuwalinda watoto.

default

Mtoto akiwa jeshini katika Vita ya Iraq na Iran

Karibu tangu miaka 20 sasa, watoto wako katika hifadhi maalum ya jamii ya kimataifa tangu mwaka 1990, ulipoanza kufanya kazi mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kuwalinda watoto. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba kuna watoto laki tatu katika nchi nyingi ambao wanatumiwa kama wanajeshi, jambo ambalo, kwa mujibu wa vipimo vya kimataifa, ni uhalifu wa kivita. Mwezi huu Ujerumani ni mwanachama asiyekuwa wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na leo, chini ya uongozi wake, mdahalo wazi utafanyika katika baraza hilo kuhusu mada hii: vipi watoto katika maeneo ya mizozo wanavyoweza kulindwa kwa njia ilio bora zaidi...

Sudan ya Kusini huenda wiki hii ikaingizwa kama mwanachama wa 193 wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kwa mujibu wa Irina Bokova, katibu mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, vita vya kienyeji vya miongo kadhaa katika nchi hiyo vimeacha alama zake. Huko Sudan Kusini, mtu anaweza kuona wazi wazi nini maana ya vita kwa watoto:

Sudan Kindersoldaten

Wanajeshi watoto wakitembea nyuma ya mwanajeshi mtu mzima wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan, SPLA, kabla ya mapatano yaamani ya nchi hiyo

"Wakati wa mzozo huo, shule na watoto wa shule walishambuliwa, tena kwa njia ya mpangilio. Sudan ya Kusini hivi sasa ina kiwango cha watoto wachache kabisa wanaokwenda shuleni duniani. Kwa wasichana, uwezekano ni mkubwa zaidi wa wao kufa wakati wa kuzaa kuliko ule uwezekano wa wao kumaliza shule. Ni asilimia nane tu ya wanawake wanaojua kusoma na kuandika. Hamna nchi ambapo inahitajika kuwekwa wazi zaidi juu ya umuhimu wa haki ya kupata masomo ya shule kama ilivyo Sudan ya Kusini."

Tarakimu zilioko duniani kote kuhusu hali kama hiyo ni za kutisha. Shirika la UNESCO linakadiria kwamba baina ya mwaka 1998 na 2008, watoto milioni mbili wameuwawa katika mizozo ya kisilaha na milioni sita wamejeruhiwa vibaya. Karibu ya watoto laki tatu wanatumiwa vibaya kama wanajeshi, huku wakibakwa.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, uhalifu wa aina sita unaangaliwa kuwa ni uhalifu wa kivita, kama vile kuwatumia watoto kama wanajeshi, kuwaamrisha wauwe au kuwatumia king'ono. Upande katika mzozo ambao unafanya uhalifu huo unaweza ukaingizwa katika orodha ya Umoja wa Mataifa inayohusu watu wakorofi. Kwa mujibu wa balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, Peter Wittig, ni kwamba jambo hilo halina dhara, lakini linaweka mbinyo.

Nchi, serikali na pia makundi ya waasi yalio na silaha yaliomo katika orodha hiyo, kwa wao ni doa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, katika kuyatayarisha majadiliano ya leo,amesema kuna mpango wa hatua 15 ambazo zinaweza kukubaliwa, hatua nyingine mbili zinaweza kungoja kukubaliwa hadi mwisho wa mwaka huu.

Ban Ki Moon kandidiert für zweite Amtszeit Flash-Galerie

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

" Mafanikio haya yanadhihirisha athari nzuri ya kuwa na orodha ya nchi korofi zisizowalinda watoto. Mfano mwengine ni Afghanistan na Chad ambako mafanikio yameonekana muda mfupi kabla ya kukubaliwa mipango hiyo. Nataka kuipongeza serikali ya Chad kwa hatua iliochukuwa ya kuwatoa watoto wote kutoka majeshi ya usalama, hivyo kuambatana na Azimio la Umoja wa Mataifa nambari 1612. Pale mpango huo wa vitendo utakapoanza kufanya kazi, Chad itatolewa kutoka ile orodha ya nchi korofi zisizolinda watoto, na nchi hiyo haitokuwemo katika ajenda ya mazungumzo ya kikundi cha kazi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Nazitia moyo serikali za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mnyanmar na Sudan, pamoja na serikali ya mpito ya Somalia, kufuata mfano huo."

Lengo la azimio ambalo litapigiwa kura leo mwanzoni mwa majadiliano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kukemea uhalifu wa aina nyingine na kutoa sababu kwa nini nchi fulani au upande fulani wa vita umetangazwa kuingizwa katika hiyo orodha ya wakorofi wasiolinda haki za watoto; kama vile kuzishambulia shule au majengo ya hospitali. Pindi azimio hilo litapitishwa, basi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika visa kama hivyo, linaweza kuchukua hatua za kuwawekea vikwazo wanaohusika.

Hadi sasa ni katika visa viwili tu ambapo hatua za ziada zilichukuliwa; miaka michache iliopita huko Cote d'Ivoire na karibuni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Licha ya hayo, sio nchi au pande zote za mizozo zinazotishika kuingizwa katika orodha ya wakorofi wanaoendea vibaya haki za watoto. Lakini wanasheria wanaopigania haki za watoto hawajakata tamaa. Na ikiwa hatua zinazopigwa sasa zikiendelea, kwa mujibu wa makisio, ni kwamba mnamo miaka 25 ijayo, angalau hakutakuweko tena watoto wanaotumika jeshini.

Mwandishi: Bergmann, Christina/Othman, Miraji/ZR

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

 • Tarehe 12.07.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11tX5
 • Tarehe 12.07.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11tX5

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com