1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika waazimia kuvimaliza vita vya Ukraine.

Zainab Aziz
17 Mei 2023

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema marais wa Urusi na Ukraine wamekubali kuutafakari mpango wa amani wa nchi za Afrika juu ya kuvimaliza vita vya Ukraine utakaowasilishwa kwao kwa nyakati tofauti.

https://p.dw.com/p/4RSuC
Südafrika | Cyril Ramaphosa
Picha: UNTV/AP/picture alliance

Rais Ramaphosa amesema ujumbe wa viongozi wa nchi za Afrika utaenda Urusi na Ukraine kwa lengo la kusaidia kuvimaliza vita hivyo. Ramaphosa alizungumza kwa njia ya simu na marais Vladimir Putin wa Urusi na Volodoymyr Zelensky wa Ukraine kwa nyakati tofauti na amesema marais hao wamekubali kuwapokea wajumbe wa Afrika kwenye miji yao, ya Moscow na Kiev ili kuujadili mpango wa kuutatua mgogoro uliopo kati ya nchi mbili hizo.

Rais wa Ukraine Volodymiyr Zelensky.
Rais wa Ukraine Volodymiyr Zelensky.Picha: president.gov.ua

Ujumbe wa Afrika utazijumuisha, Senegal, Uganda, Misri, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Afrika Kusini. Juhudi za nchi hizo za Afrika zinaungwa mkono na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na Umoja wa Afrika. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alithibitisha siku ya Jumatatu kuwa rais Ramaphosa alizungumza na Gutteres wakati wa ziara ya Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Jamaica.

Dujarric alisema Umoja wa Mataifa unapendelea na unaunga mkono mpango wowote ambao unaweza kuiongoza dunia kuelekea kwenye amani kwa kufuata Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sambamba na sheria za kimataifa na kwa mujibu wa maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Rais wa Urusi Vladimir Putin.Picha: SPUTNIK via REUTERS

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy wamekubali kufanya mikutano kwa nyakati tofauti na ujumbe wa viongozi kutoka nchi sita za Afrika kujadili mpango utakaowezesha kuvimaliza vita vya nchini Ukraine.

Chanzo:AP