Ujerumani yatupa karata yake ya pili dhidi ya Serbia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 18.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ujerumani yatupa karata yake ya pili dhidi ya Serbia

Kampuni ya China yaelemewa na maombi ya kupeleka Vuvuzela zaidi Afrika kusini

default

Kocha mkuu wa Ujerumani Joachim Löew akiwa na mchezaji tegemeo wa Ujerumani aliyezikosa fainali za mwaka huu,Michael Ballack

Wakati mashabiki wengi hapa Ujerumani na duniani kwa ujumla wakiipigia chapuo timu ya taifa ya Ujerumani kuondoka na kombe la dunia mwaka huu nchini Afrika Kusini, Kocha mkuu, Joachim Löew,amekataa kuahidi matokeo makubwa kwa kikosi hicho kilichosheheni vijana.

Ujerumani leo inatupa karata yake ya pili katika michuano ya kombe la dunia dhidi ya Serbia, ambayo imekamia kuwavurugia sherehe timu hiyo baada ya ushindi mnono wa mechi ya kwanza.

Licha ya kumkosa nahodha wake mahiri, Michael Ballack, katika michuano ya mwaka huu, Ujerumani imekuwa ikipigiwa chapuo la kulinyakuwa kombe la dunia, kufuatia kandanda safi waliyoonyesha katika mchezo wa kwanza na kuirarua bila huruma Australia mabao 4-0.

Kufuatia matokeo hayo, mashabiki hapa Ujerumani wamekuwa wakiipa nafasi ya kulitwaa kombe la dunia msimu huu, lakini Kocha mkuu, Joachim Löew, amekataa kuwaahidi mashabiki hao makubwa zaidi katika michuano ya mwaka huu, kufuatia idadi kubwa ya wachezaji wake ni kikosi cha wachezaji wadogo,waliotwaa ubingwa wa ulaya chini ya miaka 21, mwaka 2009.

Kikosi cha Ujerumani mwaka huu kinatajwa kuwa ni cha vijana wadogo zaidi katika kipindi cha miaka 76 iliyopita, hivyo kocha Löew ameeleza kuwa wachezaji wake wanajitahidi kukwepa shinikizo kubwa kutoka mashabiki wa Ujerumani ili kutoathiriwa kisaikolojia

Ujerumani, ambayo inaongoza kundi la D, ikifuatiwa na Ghana, timu pekee kutoka Afrika iliyoonja ushindi katika mechi ya kwanza dhidi ya Serbia, inatarajiwa kuteremka dimbani siku ya jumamosi dhidi ya Australia, ambapo kipa wake, Richard Kingston, anayechezea Wigan ya Uingereza, anatarajia kuibuka washindi na kuvuka kihunzi kwa kujihakikishia kuingia raundi ya pili, na kukamilisha furaha yake ya kutimiza miaka 32 siku ya jumapili.

Viungo wa Ujerumani wanaocheza soka lenye kasi na ufundi mkubwa, linawatumia zaidi wachezaji vijana na wenye ari ya ushindi, Helmut Özil, Lucas Podolski na Thomas Müller, pamoja na kipa chipukizi , Neuer, anayechezea klabu ya Schalke ya hapa Ujerumani.

Lakini mashabiki wengi wa soka hapa Ujerumani wamekuwa wakiutolea macho zaidi mtanange wa mwisho baina ya Ujerumani na Ghana, kufuatia kiungo Kevin Prince Boateng kumnyima nafasi kiungo kipenzi na nahodha wa Ujerumani, Michael Ballack, katika mechi ya fainali ya kome la FA nchini Uingereza,kwa kumchezea rafu mbaya.

Wakati macho yakielekezwa huko Afrika kusini, kampuni ya Jiying Plastic Product Corporation ya China inayotengeneza matarumbeta maarufu kwa sasa katika michuano hiyo, Vuvuzela, imeeleza kuwa sasa imeelemewa na maombi mengi ya kupeleka bidhaa hiyo nchini Afrika kusini.

Licha ya kuwepo shinikizo la kupigwa marufuku Vuvuzela katika michuano hiyo, kampuni hiyo imeuza zaidi ya vuvuzela milioni 1, na kueleza mkakati wa kutengeneza vuvuzela zaidi ya 500,000 ili kukidhi mahitaji ya mashabiki wa soka nchini Afrika kusini, ambapo Vuvuzela moja huuzwa chini ya dola moja ya Marekani.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/RTRE

Mhariri: Miraji Othman

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com