Ujerumani: Washukiwa wa itikadi kali wafikishwa mahakamani
23 Januari 2026
Washtakiwa walijiita "Kundi la Wasaksoni wanaotaka kujitenga" — kwa ufupi SS. Ilikuwa dhana ya Ujamaa wa Kitaifa: Wakati wa utawala wa kikatili chini ya Adolf Hitler kuanzia 1933 hadi mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia mnamo 1945, SS kwa urefu ilikuwa ni Schutzstaffel, kitengo maalum cha kijeshi. Kilikuwa chombo kikuu cha nguvu na muhimu katika kupanga na kutefanya mauaji ya Wayahudi na mauaji mengine ya halaiki.
Kulingana na waendesha mashtaka wa shirikisho la Ujerumani, "Wasaksoni wanaotaka kujitenga" walipanga kupindua demokrasia nchini Ujerumani miaka 75 baada ya kumalizika kwa enzi ya Kinazi. Kulingana na wachunguzi, kundi hilo linaloshukiwa kuwa la kigaidi la mrengo wa kulia lilianzishwa katika mji wa Brandis, karibu na Leipzig katika jimbo la mashariki la Saxony, mnamo 2020.
"Hili lilikuwa kundi la wanamgambo la watu wapatao 20 ambao itikadi yao iliundwa kutokana na ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Wayahudi, na kwa sehemu mawazo ya maangamizi ya dunia."
Uvamizi nchini Ujerumani, Austria na Poland
Wanaume wanane wanaodaiwa kuwa wa "Wasaksoni wanaotaka kujitenga" walikamatwa mnamo Novemba 2024 wakati wa uvamizi wa kimataifa uliofanywa nchini Ujerumani, Austria na Poland. Wamezuiliwa tangu wakati huo.
Kesi yao mbele ya Mahakama Kuu ya Mkoa katika mji mkuu wa jimbo la Saxony, Dresden, inatarajiwa kuanza Ijumaa, Januari 23, 2026.
Kulingana na upande wa mashtaka, washukiwa hao walikuwa na uhakika kwamba Ujerumani ilikuwa karibu kuanguka na katika siku flani ijayo serikali na jamii zingevunjika: "Wanachama wa shirika hilo waliazimia kutumia fursa hii kuikamata sehemu kubwa ya Saxony kwa nguvu za kijeshi kadri walivyoweza, ili kuanzisha taifa huru linalotegemea itikadi ya Ujamaa wa Kitaifa."
Kuwaangamiza na kuwafukuza
Kundi hilo linashutumiwa kupanga "kuangamizwa" kwa wawakilishi wa jimbo hilo la sasa la shirikisho la Ujerumani. Zaidi ya hayo, "SS" ilitaka "kuwaondoa" katika eneo hilo watu ambao iliwaona kuwa hawafai - hasa makabila madogo na wapinzani wa kisiasa - kupitia safishasafisha ya kikabila.
Tangu kuanzishwa kwake, "Wasaksoni wanaotaka kujitenga" wamekuwa wakipanga kila mara kwa kile walichokiona kama kupinduliwa kusikoepukika kwa mfumo huo. Waendesha mashtaka wa shirikisho wanamwona mshukiwa anayeitwa Jörg S.* kuwa kiongozi. Alikuwa na jukumu la kusimamia mawasiliano kati ya wanachama na kuongoza mafunzo ya kijeshi.