1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Ngome mpya dhidi ya ushawishi wa Urusi barani Afrika?

16 Aprili 2026

Kwa mara ya kwanza, zoezi la kijeshi la kimataifa linafanyika Libya, huku Marekani na washirika wake wakiahidi kuisaidia nchi hiyo iliyogawanyika, wakichochewa na usalama, maslahi ya kiuchumi na ushindani na Urusi.

https://p.dw.com/p/5CIpI
Libya Sirte 2026 | Zoezi Flintlock 2026 | Vikosi maalum vya Marekani na Libya vyafanya mafunzo ya pamoja
Mazoezi ya Flintlock 2026 yalianza Sirte, Libya, kwa mafunzo ya pamoja ya vikosi maalum vya Marekani na Libya.Picha: Special Operations Command Africa

Mvua nyepesi inanyesha kwenye uwanja wa kurukia ndege tunapokusanyika katika uwanja wa ndege wa jeshi wa Stuttgart kusini mwa Ujerumani. Ni saa tisa na nusu alfajiri — muda wa kuondoka.

Ndege ya Dash 8, ndege ya propela yenye injini mbili, iko tayari kupandwa. Ndege hiyo ya kijeshi itatupeleka Sirte, Libya. Mwaka 2015, ISIS iliugeuza mji huo wa pwani kuwa ngome yake kubwa zaidi nje ya Iraq na Syria.

Iliuachia tu baada ya miezi kadhaa ya mapigano makali ya nyumba kwa nyumba na vikosi vya Libya vikisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Marekani. Lakini hiyo haikuwa vita ya mwisho Sirte, kwani nchi hiyo iliingia katika vita kati ya makundi pinzani ya kisiasa.

Mazoezi ya kuunganisha vikosi vya Libya

Wiki hii, — zoezi la vikosi maalum linaloongozwa na Marekani likishirikisha mataifa 30 — limeanza hapo.

Mgeni muhimu ndani ya ndege ni John W. Brennan — jenerali wa nyota tatu na naibu kamanda wa Kamandi ya Marekani barani Afrika. Anasisitiza mara kwa mara jinsi ilivyo ya kipekee kwamba zoezi hili linawaleta pamoja wanajeshi wa Libya kutoka mashariki na magharibi ya nchi.

"Watu wa Libya wanastahili vikosi vya usalama vilivyoungana ili kuwalinda wao na maslahi yao. Usalama huleta ustawi,” anasema Luteni Jenerali Brennan.

Kwenye karatasi, Libya ni nchi moja iliyoungana. Lakini tangu mwaka 2014 imegawanyika chini ya serikali mbili pinzani. Magharibi mwa Libya inadhibitiwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, serikali ya mpito inayotambuliwa kimataifa chini ya Waziri Mkuu Abdul Hamid Mohammed Dbeibah.

Libya Sirte 2026 | Zoezi Flintlock 2026 | Viongozi waandamizi wa Uturuki, Libya na Marekani wanapiga saluti
Viongozi waandamizi kutoka Uturuki, Libya na Marekani wanatoa salamu za kijeshi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Flintlock 2026 mjini Sirte, Libya Aprili 14, 2026.Picha: Special Operations Command Africa

Utawala wa mashariki ni Serikali ya Uthabiti wa Kitaifa yenye makao yake Tobruk chini ya Waziri Mkuu Osama Hamad, inayoungwa mkono na Jeshi la Taifa la Libya chini ya Jenerali Hiftar.

Kwa nini hili ni muhimu kwa Marekani?

Baada ya miaka ya vita, pande zote mbili zilikubaliana kusitisha mapigano mwaka 2020. Hata hivyo, nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta bado imegawanyika kwa vitendo. Wanajeshi kutoka pande zote kufanya mazoezi pamoja, wakiwa wamevaa sare moja wakati wa Flintlock 2026, kunachukuliwa kuwa mafanikio makubwa.

"Libya ni eneo muhimu kwa usalama wa NATO upande wa kusini,” anaeleza Brennan kuhusu kuongezeka kwa ushiriki wa Marekani katika eneo hilo. Mashirika ya ujasusi ya Magharibi yana wasiwasi mkubwa kuhusu shughuli za makundi ya kigaidi kama ISIS na Al-Qaida katika eneo hilo.

Aidha, inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya wahamiaji wanaovuka njia ya Mediterania ya kati kuelekea Ulaya hupitia Libya kutokana na ukosefu wa udhibiti katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Kipaumbele kwa usalama wa kiuchumi

Kwa hiyo, kuleta utulivu Libya ni kulinda usalama wa ndani kwa mtazamo wa Marekani. Hata hivyo, pia ni kuhusu fursa za kiuchumi. Lengo ni kuzingatia zaidi maeneo ambapo "usalama na maslahi ya kiuchumi ya Marekani yanakutana,” kulingana na maafisa wa ulinzi wa Marekani. Utawala wa Trump una nia ya kupata rasilimali muhimu na madini katika eneo hilo. Lakini si wao pekee.

Urusi ina maslahi makubwa katika mafuta na dhahabu ya Libya. Wapiganaji wake wa kundi lililojulikana zamani kama Wagner, sasa wanajulikana kama Africa Corps, wamekuwa wakifanya shughuli nchini humo tangu 2019, wakitoa vifaa vya kijeshi na kushirikiana na Jenerali Khalifa Hiftar.

Baada ya safari ya saa tano, hatimaye tunafika Sirte. Msafara mrefu wa magari ya SUV unatuchukua hadi eneo la mafunzo. Kila baada ya mita chache, tunaona wanajeshi, polisi na magari ya kivita kando ya barabara.

Libya 2026 | Zoezi Flintlock 2026 | Naibu kamanda wa US Africa Command
Naibu kamanda wa Kamandi ya Jeshi la Marekani Afrika akishiriki katika zoezi la Flintlock 2026.Picha: Special Operations Command Africa

Ukanda mzima uko hatarini

Mazoezi hayo yana hali rahisi lakini ya kisasa: Magaidi wamewateka wahamiaji na kuwashikilia mateka. Vikosi maalum vya Libya na Marekani vinapaswa kuwaokoa na kuondoa tishio la magaidi — kazi wanayoitekeleza kwa haraka na ufanisi chini ya usimamizi wa majenerali na wageni wa heshima, akiwemo balozi wa Italia nchini Libya.

"Kwa Italia, Ulaya na Marekani, Libya iliyoungana itaweza kuleta utulivu kwa ukanda mzima,” anasema Gianluca Alberini. Akiulizwa uwezekano wa hilo kutokea, anakiri kuwa "ni mchakato,” lakini anasema "ushiriki mkubwa zaidi wa Marekani katika eneo hili ni jambo muhimu.”

Motisha za kuungana tena

Miaka miwili iliyopita, zoezi la kijeshi la pamoja kama hili halikuonekana kama jambo linalowezekana. Sasa, wakuu wa jeshi kutoka pande zote wanatoa hotuba Sirte, wakisema kuwa kuungana kwa Libya "sio chaguo, bali ni lazima.”

Jenerali Brennan anasema ukubwa wa uwekezaji unaowezekana Libya "ni motisha ya kuungana tena.” Wengine pia wanaamini hivyo, wakisema kuunganisha jeshi la Libya pia "kunapunguza nafasi kwa wahusika wengine kufanya shughuli zao bila kizuizi.”

Tigray: Safari ya kutoka kambini hadi utumwani Libya

Urusi yaongeza uwepo wake

Kuondoka kwa vikosi vya Magharibi kutoka Mali, Burkina Faso na Niger kumeacha pengo la nguvu na kuongeza ushawishi wa Urusi Sahel. Marekani na Ulaya hawataki hali hiyo ijirudie Afrika Kaskazini. Tangu 2024, Urusi imeongeza mara mbili uwepo wake wa kijeshi Afrika Magharibi na inatafuta kuimarisha ushawishi wake Libya pia.

"Uwepo mkubwa wa kijeshi wa Urusi Libya katika upande wa kusini wa NATO ni jambo linalotutia wasiwasi,” anasema balozi wa Uingereza Martin Reynolds.

Urusi inaonekana kama mdau anayefaidika katika mazingira ya machafuko.

"Tungependa kuona serikali ambayo tunaweza kufanya nayo kazi kwa karibu,” anaongeza Reynolds—serikali ambayo "haitaona haja ya kuleta nguvu za kigeni kama inavyofanyika sasa.”

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi