1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Ufaransa zatoa onyo kali dhidi ya serikali ya Ugiriki

3 Novemba 2011

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wamefanya mkutano wa dharura katika mji wa Cannes nchini Ufaransa na kutoa onyo kali kwa Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou.

https://p.dw.com/p/134Gv
Baraza la mawaziri la UgirikiPicha: picture-alliance/dpa

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wamefanya mkutano wa dharura katika mji wa Cannes nchini Ufaransa na kutoa onyo kali kwa Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou.

Wamesema nyongeza ya malipo ya euro bilioni 8 kama sehemu ya mkopo wa kimataifa itatolewa pale ambapo watu wa Ugiriki watapitisha mpango wa awamu ya pili ya mkopo iliyokubaliwa mwishoni mwa juma lililopita, katika mchakato wa kura za maoni ujao.

Mkutano huo umefanyika baada ya Papandreou sio tu kuwashangaza Merkel na Sarkozy bali kanda yote ya Umoja wa Ulaya kutokana na mpango wake wa kuitisha kura ya maoni kuhusu awamu ya pili ya mkopo wa kuikwamua nchi hiyo. Mkopo huo ulipitishwa bila kupingwa siku chache zilizopita.

Papandreou amekiri kwamba matokeo ya kura za maoni yataonesha kama Ugiriki itaendelea kuwepo katika kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya euro au la. Na amesema ana uhakika kwamba watu wa Ugiriki watapiga kura ya ndio.

Waziri mkuu huyo amesema ana matumani kwamba zoezi hilo litafanyika wiki ya kwanza ya Desemba.