Uganda yashinikizwa kuchunguza kifo cha Saidi Lutaaya | Masuala ya Jamii | DW | 10.06.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Uganda yashinikizwa kuchunguza kifo cha Saidi Lutaaya

Shirika la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Uganda itimize ahadi yake ya kuwashitaki maafisa wa usalama waliohusika katika visa vya ukiukaji wa haki za binadamu kwa kuteua afisa kuchunguza kifo cha Lutaaya

default

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Mpaka sasa, hakuna aliyetiwa hatiani kwa kifo cha mfungwa huyo Saidi Lutaaya, kilichotokea mnamo Novemba mwaka 2007. Marehemu Lutaaya alikuwa akizuiliwa na kikosi maalum cha pamoja cha kupambana na ugaidi nchini Uganda, JATT, katika kitongoji cha Kololo, jijini Kampala.

Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, limeitaka serikali ya Uganda iheshimu mahakama kuu na mara moja ifanye uchunguzi rasmi katika kifo cha raia wa Uganda, Saidi Lutaaya. Mnamo Februari 10 mwaka huu, mahakama kuu ya Uganda ilimuamuru waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo kumteua afisa mchunguzi wa vifo katika kipindi cha miezi mitatu achunguze kifo cha Lutaaya.

Mawakili wa marehemu huyo walikwenda mahakamani Desemba mwaka jana kutafuta amri ya mahakama katika uchunguzi wa kifo cha Lutaaya kwa maujibu wa sheria za Uganda. Miezi minne imepita sasa bila mtu yeyote kuteuliwa kutekeleza amri hiyo. Msemaji wa shirika la Human Rights Watch mjini Kampala, Uganda, Maria Burnett, anasema

"Tuna matumaini waziri wa mambo ya ndani atamteua afisa mchunguzi wa vifo. Katika kesi hii ameamriwa afanye hivyo na mahakama kuu ya Uganda. Tunachokitaka sasa ni waziri huyo atimize maagizo ya mahakama kuu."

Mpaka sasa haifahamiki wazi ni kwa nini serikali imechukua muda mrefu kumteua afisa wa kuchunguza kifo cha mshukiwa huyo aliyekuwa akizuiliwa na maafisa wa usalama. Bi Maria Barnett amesema ana matumaini waziri wa mambo ya ndani wa Uganda tachukua nafasi hii kumteua afisa atakayechunguza kifo cha Saidi Lutaaya kwa kuwa familia yake imekuwa gizani kwa muda mrefu bila kujua kilichosababisha kifo cha jaama yao.

Mnamo mwaka jana, shirika la Human Rights Watch liliorodhesha visa kadhaa vya kuzuiliwa wafungwa kwa njia isiyo halali, mateso na mauaji yaliyofanywa na kikosi cha pamoja cha kupambana na ugaidi cha Uganda, JATT. Haijabainika wazi ikiwa maafisa wa kikosi hicho walimkamata bwana Said Lutaaya mnamo Novemba 23 mwaka 2007, aliyekuwa akifanya kazi kama mchuuzi wa bidhaa za rejareja mjini Kampala, siku moja kabla kuanza mkutano wa viongozi wa serikali za nchi wanachama wa jumuiya ya madola.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema maafisa wa usalama walimpiga bwana huyo na nyundo kichwani, akaanguka chini na kukimbizwa hospitali ya Mulago mjini Kampala ambako madaktari walitangaza alikuwa ameaga dunia. Kwa mujibu wa wafanyakazi wa hospitali hiyo, maiti ya mhanga huyo ilichukuliwa na wanajeshi. Familia ya Lutaaya haikupata taarifa kuhusu vipi kifo hicho kilivyotokea wala kupata maiti yake kwa ajili ya kuisitiri. Msemaji wa shirika la Human Rights Watch nchini Uganda, Maria Barnett anasema

"Tunaitaka serikali itimize ahadi zake na kuchunguza kesi za ukiukaji wa haki za binadamu na kuwaadhibu wahusika. Hatutaki tu haki itendeke kwa wahanga, bali tunataka visa hivi vya ukiukaji vikome kabisa nchini Uganda"

Kaimu mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch barani Afrika, Rona Peligal, amesema kesi ya marehemu Lutaaya ni nafasi muhimu kwa serikali ya Uganda kuonyesha kujitolea kwake kwa dhati katika juhudi za kumaliza kabisa mateso yanayofanywa na vikosi vya usalama.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 10.06.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Nngd
 • Tarehe 10.06.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Nngd

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com