1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa nchi jirani na Kenya waanza kuinuka baada ya kubanwa na mgogoro wa kisiasa.

Kalyango Siraj11 Machi 2008

Kuna matumaini kuwa sasa hali ni shwari Kenya uchumi wa nchi jirani nao utaimarishwa.

https://p.dw.com/p/DMkz
Watu wanakimbilia usalama wao wakilindwa na Polisi katika ghasia za kikabila mjini Naivasha, eneo ambalo ni muhimu kwa uchumi wa mataifa jirani na Kenya kupitishia bidhaa zao kwenda na kurudi katika bandari ya Mombasa. Wakati wa mgogoro hakuna magari yalikuwa yanapita katika maeneo mengi kama hilo.Picha: AP

Uchumi wa nchi jirani na Kenya unaanza kupumua baada ya kubanwa na mgogoro wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo na kusababisha watu 1000 kuuawa huku wengine nusu millioni kuachwa bila makazi.

Hata hivyo hali ya kiuchumi ya kanda itachukua mda mrefu kurejea katika hali yake ya kawaida kutokana na sababu zingine kama vile kupanda kwa bei ya mafuta duniani .

Baada ya kutolewa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Disemba 27 mwaka jana nchini Kenya magenge ya vijana yalichoma mimea na pia kufunga barabara kuu kwa karibu wiki nzima.

Hali hiyo ilivuruga usambazaji wa mafuta,chakula na bidhaa zingine ndogondogo kwa mataifa jirani ambayo hayana upenyo wa bahari kuu kama vile Uganda,Rwanda, Burundi.Kishindo hicho pia kiliyapata maeneo kadhaa ya nchi za jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na vilevile maeneo ya Kusini mwa Sudan.

Lakini,kupunguka kwa ghasia mwezi wa Febuari na badae kupatikana kwa mapatano ya kugawana madaraka kumebadilisha hali ya mambo.

Sasa mizingo imeanza kupitia Kenya hadi inakohitajika.Kenya tangu ijipatie uhuru mwaka wa 1963,imekuwa mlango wa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki pamoja na Afrika ya kati.

Mhadhiri wa masuala ya kiuchumi katika chuo kikuu cha Nairobi-Jasper Okello-ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa uchumi wa kanda umekumbwa na matatitizo yasiokwisha.Upande mmoja bei za vitu katika soko la kimataifa zimepanda,tena mitandao ya usafiri nchini Kenya kuelekea sehemu za ndani na nje yake imevurugwa.

Mataifa mengine, kama ilivyo Kenya yanasema kuwa shabaha za viwango vya ukuaji wa kila mwaka wa uchumi wake,ambavyo vimekuwepo katika kanda hii katika kipindi kilichopita ,visingeathirika kutokana na kipindi kifupi cha matatizo kwani mihimili ya uchumi baado ipo imara.

Rwanda na Tanzania zinakadiria viwango vyao vya ukuaji wa uchumi wake ni zaidi ya asili mia saba huku Uganda kwa upande wake inakadiria asilimia 6.9.

Mtumishi wa wizara ya Fedha ya Uganda, Keith Muhakanizi,amenukuliwa akusema kuwa,wiki za mwisho za miezi ya Febuari Machi zinaonyesha kama hali inarejea kuwa ya kawaida.

Wataalamu wa mambo ya uchumi wanasema kuwa kishindo kwa uchumi hapo baadae kitakuwa kupanda kwa bei za bidhaa duniani pamoja na bei za mafuta katika soko la kimataifa.

Bei ya pipa moja la mafuta ni dola 100 na hali hii itasababisha mfumuko wa bei katika kanda hiyo.

Mfumuko wa bei nchini Tanzania na Rwanda ulipanda katika bei za mafuta na ya vyakula tangu mwisho wa mwaka wa 2007.

Katika hali ya kueleza kupanda kwa bei ya bidhaa,mkurugenzi wa baraza la nafaka la Afrika Mashariki- Anne Mbaabu amesema bei ya sasa ya mahindi inaifaidi sana Uganda.

Amesema kuwa kawaida bei ya tani moja ya mahindi ingekuwa dola 150 lakini sasa ni dola 184.

Wakati wa mgogoro wa Kenya, wataalamu wa masuala ya uchumi walionya kuwa Uchumi wa kanda ya Afrika Mashariki mtiririko wa mapato kwa mataifa ya kanda uliathirika.

Wakati huo magenge ya vijana yaliweka vizuizini barabarani na wakati mwingine mizigo iliibwa.Hali hiyo ililamisha mataifa kadhaa kuhama kutoka bandari ya Mombasa na kuhamia bandari ya Dar-es- salaam.

Lakini huko nako kuna hasara zake.

Wizara ya fedha ya Rwanda inasema kuwa gharama ya malori ya mizigo kutoka Mombasa hadi Kigali ni dola 244 kwa wastani kwa kila tani huku kutumia bandari ya Dar-es-salaam gharama huwa ni dola 400.

Burundi inasema kuwa mgogoro wa Kenya uliisababishia hasara ya dola millioni tatu kila mwezi kupitia kodi kutokana na gharama ya juu ya kuagiza vitu kutoka nje.

Wataalamu wa uchumi pamoja na wafanya biashara wanasema kuwa athari za mgogoro huo kwa uchumi wa nchi za kanda hiyo,zitakuwa za mda mfupi ikiwa biashara itarudia kuwa ya kawaida kama kabla ya mgogoro huo.