1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi asisitiza msimamo wake wa kutozungumza na M23

Saleh Mwanamilongo
29 Aprili 2024

Kwenye mahojiano maalumu na DW rais wa Kongo Felix Tshisekedi amesema kikwazo kwa amani katika kanda la Maziwa Makuu ni jirani yake rais wa Rwanda Paul Kagame.

https://p.dw.com/p/4fIAo
Marais Paul Kagame wa Rwanda, Joao Lourencou wa Angola na Felix Tshisekedi wa Kongo
Marais Paul Kagame wa Rwanda, Joao Lourencou wa Angola na Felix Tshisekedi wa KongoPicha: JORGE NSIMBA/AFP

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekutana mjini Berlin Jumapili jioni  na rais wa Kongo Felix Tshisekedi na kuzungumzia hali ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi nchini Kongo. Tshisekedi amewatolea wito wawekezaji kutoka Ujerumani kuwekeza nchini mwake.

Mkutano huo wa ana kwa ana baina ya Rais Tshisekedi na Kansela Scholz uliodumu kwa muda wa saa mbili ulifuatiwa na chakula cha jioni baina ya viongozi hao wawili. Taarifa ya ofisi ya Kansela Olaf Scholz imesema Ujerumani inaunga mkono juhudi za upatanishi wa mzozo wa Kongo zinazofanywa na rais wa Angola, Joao Lourencou.

Mahusiano ya panda shuka na Rwanda

Kwenye mahojiano maalumu na DW, kando ya ziara yake, rais Félix Tshisekedi anasema yuko tayari kwa mazungumzo na rais wa Rwanda Paul Kagame, huku akitupilia mbali uwezekano wa mazungumzo na kundi la waasi la M23.

''Nimekuwa nikisema kila mara kwamba siwezi kamwe kukutana na waasi wa M23, sababu ni moja pekee : Ni vibaraka ambao walitengenezwa kwa ajili ya kuhalalisha uvamizi dhidi ya nchi yangu ya Kongo. Lakini kiuhalisia, mvamizi halisi, mhalifu halisi, ni Paul Kagame. Na ninataka kukutana naye sio kwa lengo la kumsihi  au kujadiliana naye chochote, bali kwa ajili ya kumwambia wazi, ana kwa ana, kwamba yeye ni mhalifu, na lazima asitishe.", alisisitiza Tshisekedi. 

Tshisekedi amesema anazingatia pia miito iliyotolewa na nchi washirika wa Kongo kwa ajili ya kuweko na usitishwaji mapigano ili kuipa nafasi juhudi ya kutafuta amani.

''Kongo iwe mfano wa maendeleo ya Afrika''

Kongo mwanachama wa nchi 13 za mpango wa Compact with Afrika
Kongo yaingia kuwa mwanachama wa 13 wa Compact with AfrcaPicha: Kay Nietfeld/picture alliance

Akizungumzia uwekezaji nchini mwake Tshisekedi amepengoza kuteuliwa kwa nchi yake kama mwanachama wa mpango wa kukuza uwekezaji mkubwa wa kibinafsi barani Afrika, Compact with Africa, unaozileta pamoja nchi 13 za Afrika pamoja na wawakilishi kutoka mataifa makubwa ya kiuchumi ya G20.

Mpango huo wa ushirikiano na Afrika unasimamiwa na Ujerumani. Hata hivyo, Tshisekedi amesema ndoto yake ni kuona Ujerumani inachangia katika uwekezaji mpana nchini Kongo.

''Ninachokifikiria ni ushirikiano mpana na Ujerumani, kwa mfano katika kile tunachohitaji sana, yaani miundombinu. Ninavutiwa sana na kile kinachofanywa hapa Ujerumani. Nimekuwa nikisema kwamba nina ndoto ya kuifanya nchi yangu kuwa aina ya 'Ujerumani ya Afrika', inaamanisha Kongo iwe mfano wa maendeleo ya Afrika.'', alisema Tshisekedi.

Ziara hii ya Rais wa Kongo Felix Tshisekedi barani Ulaya inampeleka pia nchini Ufaransa ambako ametarajiwa kukutana na Rais Emmanuel Macron, kabla ya kufungua mkutano wa kiuchumi baina ya wafanya biashara wa Kongo na Ufaransa baadae kesho.