Trump achoshwa na mikutano isiyoleta mwanga wa amani Ukraine
12 Desemba 2025
Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House Karoline Leavitt amesema Rais Donald Trump "amechoshwa na mikutano ya mara kwa mara" ambayo haijatoa mwanga wa kufikia makubaliano ya kuvimalita vita kati ya Urusi na Ukraine.
Ametoa kauli hiyo wakati Kyiv ikieleza kwamba Washington bado inaishinikiza ikubali mpango wake unaojumuisha kuachia baadhi ya maeneo yake kwa Urusi kama sehemu ya makubaliano ya kuvimaliza vita vilivyodumu takriban miaka minne.
Leavitt amewaambia waandishi wa habari kwamba Trump hataki tena kile alichokiita maneno matupu bila vitendo na kwamba anachotaka kuona sasa ni vita hivyo kufika mwisho.
Hivi karibuni, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitoa kauli iliyoashiria kwamba hakuna mabadiliko makubwa katika msimamo wa Marekani juu ya namna vita hivyo vinapaswa kumalizika tangu Washington ilipowasilisha mpango wake wa vipengele 28 mwezi uliopita - mpango ulioonekana kuipendelea zaidi Urusi.
Zelensky afichua shinikizo la Marekani
Zelensky ameweka wazi kuwa Marekani bado inaishinikiza Ukraine kuikabidhi Urusi maeneo yake kadhaa kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza vita vilivyoanza Februari mwaka 2022.
Kiongozi huyo amewaambia waandishi wa habari kwamba "Washington inaitaka Ukraine pekee na wala sio Urusi, iondoe wanajeshi wake kutoka maeneo ya mashariki mwa Donetsk, sehemu ambayo eneo huru la kiuchumi lisilo na vikosi vya usalama lingeanzishwa kama kizuizi kati ya majeshi ya nchi hizo mbili.”
Kulingana na mpango mpya wa Marekani, Urusi pia ingebaki na maeneo inayoyashikilia kusini mwa Ukraine, lakini ingelazimika kuondoa baadhi ya wanajeshi wake katika maeneo ya kaskazini ambayo Rais wa Urusi Vladimir Putin hajadai kuyakamata.
Ukraine imekuwa ikipitia upya pendekezo la awali la Marekani, na wiki hii iliwasilisha pendekezo jipya kwa Washington lenye vipengele 20, ambalo hata hivyo maelezo yake yote bado hayawekwa wazi.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema kuwa "wiki ijayo itakuwa muhimu” katika kutafuta amani ya haki na endelevu kwa Ukraine.
Ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa X na kuonya kwamba, makubaliano yoyote ya amani hayapaswi kuacha mianya ya mgogoro wa baadae na kuhatarisha usalama wa Ulaya.
Rais wa Marekani Donald Trump kwa kiasi kikubwa ameonekana kuipiga kumbo Ulaya katika mchakato huo wa amani na badala yake kufanya mazungumzo moja kwa moja na Urusi na Ukraine, kupitia juhudi za kidiplomasia zilizoongozwa na mjumbe wake Steve Witkoff, na hivi karibuni mkwe wake Jared Kushner.
Wakati huo huo, Ukraine inasisitiza kuwa na nguvu ya askari 800,000 katika jeshi lake chini ya pendekezo lililoboreshwa la mpango wa amani.
Zelensky amesema kuwa rasimu ya sasa yenye vipengele 20 imefanyiwa marekebisho ya kutosha.
Mpango wa awali wa Marekani, uliowekwa wazi mwezi Novemba, uliipangia Ukraine kikomo cha askari 600,000.
Hata hivyo, wachambuzi wameonyesha mashaka kuhusu uwezo wa Ukraine kufikia idadi hiyo. Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka, kumekuwa na zaidi ya matukio 300,000 ya askari kutoroka au kutohudhuria kazini tangu uvamizi wa Urusi..
Kabla ya vita hivyo kuanza, Ukraine ilikuwa na jeshi la kudumu lenye takriban askari 290,000.
Ili kufidia upungufu wowote wa wanajeshi, Kyiv inatarajia washirika wake wa Magharibi kuchangia kuongeza nguvu ya kijeshi endapo makubaliano ya amani yatafikiwa.